TADB yaahidi kuwapatia mikopo wakulima wa zabibu
Na Abdallah Luambano, Dodoma
Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), imewahakikishi wakulima wa zao la zabibu kupata mikopo itakayosaidia uzalishaji wa zao hilo ambalo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati na muhimu kwa utoaji wa malighafi ya kutengenezea mvinyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano na wadau wa zao hilo ulioitishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine amesema benki yake itaendelea kutekeleza mikakati ya serikali ya kukuza sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji na kuwaunganisha wakulima wengi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao.
“Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa kwa benki hii ni pamoja na kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mapinduzi yenye tija katika sekta ya kilimo nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa mikopo. Tunawahakikishia wakulima wa zabibu mikopo yenye masharti nafuu na ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo muhimu,’’ alisema Bw. Justine.
Bw. Justine amewataka wakulima kuondoa hofu ya kukosa mikopo kwa kigezo cha kukosa dhamana kwani kinachomfanya mkulima akopeshwe na benki hiyo ni uwezo wa mradi husika.
“TADB huwa tunatumia dhamana kama sehemu ya kupunguza makali pale ambapo deni litakaposhindikana kulipwa, hivyo nawaomba wakulima kuacha kufikiria juu ya dhamana,’’ alisema Bw. Justine.
Aidha aliishukuru serikali kwa namna ilivyorahisisha zoezi la upatikanji wa mikopo kupitia TADB kwa kutoa pesa kiasi cha shilingi bilioni 55 kama sehemu ya dhamana ili kumrahisishia mkulima mdogo aweze kukopesheka na benki pamoja na mabenki washirika.
“ Tunaishukuru serikali kupiti Ofisi ya Waziri Mkuu ilipoona wakulima wadogo na wa kati wanashindwa kufikia asilimia 50 ya dhamana, ikatoa kiasi cha dola za marekani milioni 25 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 55 za kitanzania ambapo kupitia TADB wanaweza kudhaminika na mabenki washirika,’’ alieleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI), Dkt.Geofrey Mkamilo amesema kunaupungufu katika uzalishaji wa miche ya zababu na kwamba wataendelea kufanya tafiti za mbegu bora zaidi na kuzizalisha kwa wingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya ndani.
“Tumeweka mkakati wa kuendelea kuzalisha miche bora kwa njia ya tone na chupa ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa mbegu ambapo kwa Dodoma pekee zinahitajika takribani miche bilioni 5.6 zitakazopandwa kwenye eneo la hekta milioni 2.1 ambazo zinafaa kwa kilimo cha zabibu,’’ alisema Dkt. Mkamilo
Awali wakati akihutubia
mkutano huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka wadau na Taasisi zote
zinazojihusisha na sekta ya kilimo ikiwemo TADB, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
(TARI) pamoja na Asasi ya kusaidia sekta binafsi ya kilimo (PASS) kuendelea na
kampeni iliyoanzishwa na serikali ya kuhimiza kilimo cha zabibu kwa kumsaidia
mkulima kuanzia maandalizi ya shamba, upatikanaji wa pembejeo hadi hatua ya
mauzo.
Mwisho.
Comments
Post a Comment