SADC yaviamsha viwanda vya Tanzania kuchangamkia masoko nje
SADC yaviamsha viwanda vya Tanzania kuchangamkia masoko nje
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MKUTANO wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) umeamsha ari ya viwanda vya Tanzania kupanua wigo wa kibiashara
kwa kuongeza uzalishaji ili bidhaa za ndani na kutafuta masoko katika
nchi wanachama wa jumuia hiyo.
Ari hiyo imeibuka mwishoni mwa wiki, baada ya ujumbe wa SADC uliopo
nchini, kufanya ziara katika kiwanda cha kutengeza vifungashio cha
Global Packaging Limited kilichoko Kibaha, mkoani Pwani.
Akitoa maelezo kwa wajumbe kiwandani hapo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Global Packaging (T) Limited, Bwana Benno Mwitumba, alisema kiwanda
chake kimepanga kupanua wigo wa uzalishaji kwa kuanzisha awamu
nyingine ya upanuzi wa kiwanda kwa lengo la kuongeza uzalishaji, huku
masoko yakitafutwa zaidi kwenye nchi nyingine za SADC.
Bwana Mwitumba amesema kiwanda hicho ambacho kilizinduliwa na Rais
John Magufuli Juni mwaka 2017, kimesaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza
uzalishaji wa vifungashio kukidhi soko la ndani, na sasa mkakati ni
kukipanua kiwanda pamoja na uzalishaji ili kuweza kukidhi mahitaji ya
soko katika nchi za SADC
“Miaka hii miwili tumepata mafanikio makubwa na uzalishaji na tunataka
kuingia katika awamu ya tatu ya upanuzi wa kiwanda chetu baada ya
kupata hamasa kubwa ya uwepo wa soko kwenye nchi wanachama wa SADC,”
alisema Bwana Mwitumba.
Alisisitiza kuwa “Tunakusudia kwamba baada ya kukamilisha upanuzi huo,
tutaweza kuuza vifungashio hivi nje na hasa tukiliwania Zaidi soko
lililopo kwa wenzetu ndani ya SADC, na kwa msaada wa serikali yetu
tunaamini azma yetu itatimia.”
Aidha Mkurugenzi huyo ameziomba taasisi za serikali zinazohusika
katika uwekezaji, kutoa huduma kwa haraka pasipo urasimu kwa
wawekezaji, ili jitihada za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda
iweze kukamilika kama ilivyokusudiwa na serikali.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa
(NDC) Profesa Damian Gabagambi, alisema NDC kama mwanahisa kwenye
kiwanda hicho cha Global Packaging Limited, inaona fursa kubwa iliyopo
ya masoko katika nchi za SADC, na hivyo itahakikisha azma ya upanuzi
inafanikiwa na soko la uhakika kutafuntwa kwenye nchi hizo.
“Kwa sasa uzalishaji wetu ni vifungashio vidogo milioni 25 kwa mwaka
ama vikubwa milioni 17, tunakusudia upanuzi wa kiwanda utasaidia
kuongeza uzalishaji mara tatu Zaidi, na hivyo kupenya kwa nguvu zote
katika soko la nchi za SADC”, alisema Profesa Gabagambi.
Aliongeza kuwa mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali ya
awamu ya tano, yamesaidia kuwepo na mafanikio makubwa kwenye sekta ya
viwanda, hatua itakayochochea ushindani wa kweli kwenye soko la
kimataifa.
Naye kiongozi wa ujumbe wa SADC uliyotembelea kiwanda hicho Bwana
Gastom Kaziri, alikipongeza kiwanda hicho kwa kuwa na teknolojia ya
hali ya juu, ambayo inafanya kiwanda kizalishe vifungashio vingi kwa
muda mfupi, huku vikiwa na ubora wa kimataifa.
“Global Packaging ni mfano wa kampuni zinazotumia teknolojia kubwa, na
kwa hatua mliyofikia sasa, ni vema mkatoka nje ya Tanzania hata
ikibidi kujenga viwanda nje ama kutafuta masoko ya bidhaa zenu huko
nje ya nchi”, alisema Bwana Kaziri.
Mmiliki wa Wande Printing and Packaging (T) Ltd ambao ni wanahisa
katika kampuni ya Global Packaging (T) Ltd, Bwana Joseph Wasonga,
alielezea kuwa harakati za upanuzi wa kiwanda zinakwenda vizuri, huku
akipongeza ushiriki wa taasisi za kifedha katika kufanikisha jitihada
za ujenzi wa Tanzania ya viwanda.
Ujumbe wa SADC ambao upo nchini kwa ajili ya vikao vya awali kabla ya
mkutano wa wakuu wanchi za jumuia hiyo, ulitembelea kiwanda hicho cha
vifungashio kilichopo Kibaha mkoani Pwani, ili kujionea teknolojia ya
hali ya juu ambayo inatumiwa na viwanda vya Tanzania katika uzalishaji
wa bidhaa mbalimbali.
Kiwanda cha Global Packaging (T) Limited kinamilikiwa kwa ubia baina
ya kampuni ya Wande Printing and Packaging (T) Ltd pamoja na Shirika
la Maendeleo la Taifa (NDC).
Mwisho.
Comments
Post a Comment