TADB: Wakulima Kunufaika na Dhamana ya mikopo kwa asilimia 50%



Na Mosses Ferdinand, Dar es salaam,

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewahakikishia dhamana ya asilimia hamsini (50%) wakulima ili kuwawezesha kuweza kupata mikopo itakayoweza kuwezesha ufanisi katika sekta ya kilimo.

 

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 20 na Mfuko wa Dhamana Afrika (AGF), Makao Makuu ya Benki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw. Japhet Justine amesema Benki imeingia makubaliano hayo kwa lengo la kuwainua wakulima wadogowadogo, wa kati na wakubwa ili kuwawezesha uarahisiwa kupata mikopo kwa kupata dhamana nafuu.

 

“Leo tumefikia makubaliano haya na wenzetu wa AGF yenye malengo mazuri kwa wakulima wetu kwa maana kurahisisha kupata dhamana ya asilimia hamsini pindi waombapo mkopo” Alisema Bw. Japhet.

 

Amesema makubaliano hayo yamejikita pia kwenye kuwasaidia wanawake kwa kuwa sehemu kubwa ya watu wanaofanya shughuli za kilimo nchini ni wanawake.

 

“Wote tunafahamu kuwa vijana wengi hawajachangamka sana kujishughulisha na kilimo, hivyo tumeona ni fursa kwetu kupitia makubaliano haya ambayo moja kwa moja yatawasaidia wanawake kwa kiasi kikubwa”.

 

Kwa upande wake, akimwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango Bw. Mwigulu Nchemba, Kamishna Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja amepongeza makubaliano hayo na kusema yamekuja wakati muhafaka pindi ambacho serikali imetoka kupitisha Mpango wa tatu (3) wa Maendeleo nchini ambao umeuipa kipaumbele sekta ya kilimo.

 

“Kwa dhati nichukue fursa hii kupongeza makubaliano haya yenye lengo zuri kwa maendeleo ya Sekta ya kilimo kama ilivyoainishwa kwenye vipaumbele vya Kwenye Mpango wa tatu wa Maendeleo uliozinduliwa na serikali hivi karibuni”. Alisema Dkt. Mwamwaja.

 

Aliongeza kuwa kwa miaka ya karibuni kumekuwa na changamoto kubwa ya kupata dhamana kwenye mikopo hivyo makubaliano hayo yataenda kuwasaidia wakulima na kurahisisha namna ya kupata mikopo kwa urahisi.

 

“Makubaliano haya yatafungua njia ya kuweza kupata mikopo kwa urahisi  na kupunguza changamoto kwenye kupata udhamini pindi watakapoomba mikopo kwa ajili ya shughuli za kilimo”.

 

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Dhamana Afrika (AGF) Jules Ngankam amesema makubaliano hayo yatawazesha wakulima kuweza kupata dhamana ya mikopo yao jambo ambalo litawezesha kuweza kulima kwa tija na kuacha desturi ya kuagiza chakula kutoka nje.

 

“Afrika tumekuwa tukiagiza chakula takribani asilimia kumi (10), kutoka nje kutokana na kilimo duni, hivyo makubaliano haya yatasaidia kuongeza tija kwa wakulima kulima kwa tija ili kuweza kujitegemea kwa chakula chetu wenyewe”. Alisema Bw. Ngankam.

 

Amesema mbali ya changamoto ya ugonjwa wa uviko 19 ulioikumba Dunia, bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha sekta ya kilimo inakua kwa kuwa ni sekta nyeti yenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta zingine kama vile viwanda na biashara.

  

“Kwa sasa kumekuwa na changamoto kubwa kutokana na athari za ugonjwa wa Uviko 19 Duniani, ila hatuna budi kujidhatiti kuhakikisha sekta hii inaimarika kutokana na mchango wake kwenye maendeleo ya sekta nyingine”.

 

Kwa kiasi kikubwa hii ni hatua kubwa kwa maendeleo ya sekta kilimo kwa kuwa wakulima wataweza kupata dhamana ya mikopo na kurahisisha kufanya kilimo chenye tija.

 

Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

NEMC warns on emptying effluent in built-up areas, flood waters

Set aside land for investment, Kairuki tells RCs,district councils