TNBC kufanyia kazi mapendekezo ya wataalam kuhusu mazingira ya biashara

Balozi wa Sweden nchini Tanzania Bw.Anders Sjoberg(kushoto) akishirikia zoezi la uzinduzi wa repoti ya hali ya biashara na uwekezaji kwa makampuni ya Nordic yaliyopo nchini na kuikabidhi kwa Serikali ili ifanyiwe kazi. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) Dkt.Godwill Wanga na katikati ni Katibu Mtendaji wa  Taasisi ya Utafiti wa Sera na Maendeleo (REPOA) Dkt.Donald Mmari.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) Dkt.Godwill Wanga (katikati),akizungumza jambo na waandishi wa habari kwenye hafla ya uzinduzi wa repoti ya mazingira ya Kibiashara kwa makampuni ya Nordic nchini Tanzania na kuahidi kuwa watakwenda kufanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza ili kuchochea uwekezaji na biashara nchini. kulia ni Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Sera na Maendeleo(REPOA) Dkt.Donald Mmari  na kushoto ni Balozi wa Sweden Nchini Tanzania Bw.Anders Sjoberg.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC)Dkt.Godwill Wanga (kushoto) akizungumza jambo na Balozi wa Sweden Nchini Tanzania Bw. Anders Sjoberg(kulia) mara baada ya kumalizika kwa hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya mazingira ya Biashara ya Kampuni za Nordic nchini Tanzania.


Na Abdallah Luambano, Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la Biashara (TNBC) limepokea ripoti iliyoandaliwa na Taasisi  ya Utafiti ya REPOA kwa kushirikiana na nchi za Sweden,Denmark, Norway na Finland inayoeleza hali ya uwekezaji na mazingira ya biashara kwa nchi hizo hapa nchini na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyomo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya ripoti hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam,  Katibu Mtendaji wa wa TNBC, Dkt Godwill Wanga alisema kuwa tafiti zenye weledi zinazoelezea hali ya mazingira ya biashara na uwekezaji zinachagia kwa kiasi kikubwa katika kutatua changamoto zilizopo na kuweka mazingira mazuri zaidi ya kibiashara.

“Leo tumepokea ripoti kutoka REPOA ambayo inaeleza namna serikali ilivyofanikiwa kuweka mazingira rafiki na kuwezesha biashara na uwekezaji pamoja na kutaja maeneo ambayo bado changamoto,’’ alisema Dkt. Wanga na kuongeza kuwa serikali imedharia kuhakikisha kuwa mazingira ya biashara yanaendelea kuimarika na kuvutia wawekezaji zaidi.

Dkt. Wanga alisema kuwa licha ya jitihada kubwa zilizochukuliwa na serikali katika kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara Tanzania, zipo baadhi changamoto  ambazo  serikali kupitia Baraza  zinaendelea kuzifanyia kazi.

“Kumekuwepo na jitihada kubwa za serikali katika kuweka mazingira rafiki ya biashara ikiwemo punguzo la tozo mbalimbali pamoja na ushirikiano wa serikali na sekta binafsi.Pamoja na hayo  yote mazuri changamoto  hazikosekani hivyo kupitia baraza  zitaendelea kutatuliwa ,’’ alieleza.

Ameahidi kuwa serikali itafanyia kazi ripoti hiyo kwa kupata majibu ya chagamoto zilizopo hasa kwenye upande wa kodi, uhamiaji hasa upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi hapa Tanzania, ubora wa bidhaa pamoja na utaalam.

Kwa Upande wake Balozi wa Sweden nchini Tanzania Balozi Anders Sjoberg alisema, licha ya changamoto zilizopo wataendelea kuita wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa mazingira yanayojengwa sasa ni mazuri lakini sababu nyingine ni mahusiano mazuri kihistoria baina ya nchi hizo.

“Mazingira ya biashara Tanzania ni mazuri licha ya changamoto zilizopo, tunaamini watu wetu wataendelea kuja kuwekeza na kufanya biashara kwa kuwa kumekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania lakini pia kwa hatua ambazo zinachukuliwa na serikali katika kuweka mazingira mazuri ya biashara,’’ alisema Balozi Sjoberg.

Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dkt. Donald Mmari alisema taasisi yake itaendelea kufanya tafiti zenye weledi mkubwa ili kuisaidia serikali iweze kufikia malengo ambayo imejiwekea.

‘’Ripoti imeonesha maeneo mbalimbali ambayo serikali imefanya vizuri na pia tumeonesha changamoto ambazo tunaamini zikifanyiwa kazi mazingira ya biashara yatakua na tutawaleta pamoja wadau wa maendeleo (serikali na sekta binafsi,’’ alisema Dkt. Mmari.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa nchi za Nordic zimewekeza katika sekta zaidi ya 20 zikiwemo viwanda na mawasiliano na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji ajira na kukuza uchumi wa Tanzania.


Comments

Popular posts from this blog

Gold mine in Songwe wins ministerial praise for protecting environment

Tanzania praised for being keen on fertilisers going to farmers

Kirenga: Kipaumbele chetu ni mkulima mdogo kupata soko la uhakika