Waziri Biteko asisitiza zebaki kutotumika migodini


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka  akizungumza  wakati wa kufunga maadhimisho ya siku tatu ya miaka 50 ya taaluma ya jiolojia  iliyofanyika mwishoni mwawiki jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nishati na Madini Dotto Biteko  akizungumza  wakati wa kufunga maadhimisho ya siku tatu ya miaka 50 ya taaluma ya jiolojia  iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.


Waziri Biteko asisitiza  zebaki kutotumika migodini

Na Abdallah Luambano, Dar es Salaam

MATUMIZI ya zebaki katika uchimbaji wa madini  umeelezwa kuwa hatarishi kwa afya ya binadamu  hasa kwa watumiaji ambao ni wachimbaji
  wadogo wa madini pamoja na mazingira yanayoizunguka eneo husika.

Akizungumza wakati wa kufunga Maadhimisho ya Siku Tatu ya Miaka 50 ya Taaluma ya Jiolojia  mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Bw.Doto Biteko alisema wizara imeingia mkataba unaozuia matumizi ya zebaki duniani kwani  ni kemikali ambayo si rafiki kwa afya ya mwanadamu pamoja na Mazingira yanayozunguka.

"Saidieni katika kuhakikisha umoja wenu unasaidia taifa hasa katika kutunza rasilimali zetu. Tuungane na serikali kuhakikisha madini yetu yanachimbwa kihalali huku tukizingatia usalama wa wachimbaji, watu wanaowazunguka na Mazingira kwa ujumla ili kuleta tija kwa nchi yetu,”
alisema.

 Alisema jiolojia ni moja ya taaluma inayogusa karibia nyanja zote za maisha na kuwaomba wanajiolojia kushirikiana na serikali katika kuhakikisha mbadala wa zebaki unasisitizwa Kama njia moja wapo ya kupunguza athari ambazo zingepelekea uharibifu wa Mazingira.

Waziri Biteko alisema taaluma ya jiolojia ni muhimu sana hasa katika sekta ya madini kwani  sekta  hiyo  ni muhimu kwa ajili ya uchumi wa nchi  hivyo kuna kila sababu ya wanajiolojia kufanya kazi zao kikamilifu na kuunga mkono azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Uchumi wa Kati na viwanda ifikapo 2025.

"Nendeni mkawe chachu ya mabadiliko ya sekta hii kwa manufaa ya nchi yetu na sio kwa manufaa binafsi. Mkawe waaminifu katika kazi zenu bila hivyo mtakua mnakwamisha watanzania wenzenu hasa wale wanaojipinda kuhakikisha wanapata mitaji ya kuwawezesha kufanya uchimbaji wa madini kikamilifu" Aliongeza Waziri Biteko.

Aidha, Waziri Biteko alisema NEMC watatangaza kipindi cha mpito juu ya matumizi ya Zebaki na kuwataka wadau kutoa ushirikiano stahiki.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka alisema matumizi ya zebaki katika uchimbaji wa madini ni hatari kiafya na serikali haiwezi kuacha watu wake wakapoteza maisha kwasababu yakupata faida.

 Dkt. Gwamaka ambaye pia  ni mhandisi alisema  serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ina lengo la kuwafanya wachimbaji wadogo kukua na kuwa wachimbaji wakubwa.
.
"Tutatafuta njia mbadala ili wachimbaji wadogo  waachane na matumizi ya zebaki na afya zao kuimarika zaidi na kufaidika na kile wanachokivuna. Hatutaki ifike mahali tuwe na matahira wengi na watu wenye utindio wa ubongo." alisema Dkt. Gwamaka,

Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kuwa kuna tatizo kubwa katika mbinu bora za uchimbaji hivyo kuchangia  ajali nyingi zaidi katika migodi na hasa utumiaji wa vitendea kazi duni katika uchimbaji.

"Kuna umuhimu wa kuwapa elimu iliyojitosheleza ya kijiolojia kwa
wachimbaji wadogo wa madini. Bila hivyo tutaendelea kuwa na ajali hadi
hapo tutakapopata njia ya kuwasaidia wachimbaji wadogo,” alisema.

Dkt. Gwamaka a ni mhandisi wa masuala ya jiolojia alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya wachimbaji wadogo wa madini na mazingira na hivyo alisisitiza kuboreshwa kwa uchimbaji ili uwe wa tija ili kila mtanzania aweze kufaidika na uchimbaji huo endelevu.

Kwa upande wake,  Kamishna Msaidizi wa Madini (Uendelezaji Wachimbaji Wadogo), Bw. Francis Mhiayo alisema  mabadiliko ya sheria ya uchimbaji wa madini ulizingatia wachimbaji wadogo na mifumo mizuri ya kuwasaidia.

“Kwasasa tunaangalia namna ya kuboresha ruzuku kama ni kuwapa vifaa moja kwa moja au la… kikubwa  zaidi tuwawezeshe katika kuwapa taarifa muhimu." Bw. Mhiayo alisisitiza.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Jiolojia kutoka GST, Bw. Maruvuko Msechu alisema idara yake  imejipanga vyema katika utoaji wa taarifa au elimu ya jiolojia, hasa juu ya matumizi ya zebaki katika uchimbaji wa madini.

 "Kama huna elimu au taarifa ya jiolojia uchimbaji unakua mgumu sana na hatarishi. Lazima tujue nchi yetu inaenda wapi. Kumekua na imani potofu, mtu anasema kalogwa na ni mmoja kati ya watu wanaotumia zebaki katika uchimbaji na baada ya muda anaanza kuumwa. Serikali inaangalia namna bora ya kuboresha maisha ya watanzania." Bw. Msechu aliongeza.

Comments

Popular posts from this blog

NEMC warns on emptying effluent in built-up areas, flood waters

Set aside land for investment, Kairuki tells RCs,district councils