DC: Tumia mbolea kunufaika na uchumi wa kati
Na Abdallah Luambano, Kigoma
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Samson Anga amewaomba wakulima wa wilaya na mkoa wa Kigoma watumie mbolea ya bure ambayo imetolewa na Yara kuinua kilimo ili wawe wanufaikaji wa kweli wa uchumi wa kati.
“Nawaomba wakulima wetu wote wachangamkie fursa hii; mbolea ni ya bure.
Tukitumia mbolea hii kwa mafanikio mazao yataongezeka, tutakuwa na hakika
ya chakula na tutakuwa sehemu ya uchumi wa kati wa taifa letu,” ameeleza DC
Anga.
Mkoa wa Kigoma una wanachi wapatao 2,305,894 (makadirio ya 2015). Ardhi
inayolimwa ni hekta 1,058,637 au asilimia 57.7 ya ardhi yote
inayofaa kwa kilimo. Mkoa unapata mvua nzuri kati ya milimita 600-1,000
kwa mwaka na mazao ya chakula ni mahindi, muhogo, mtama, viazi, ndizi na
maharage. Mkoa wa Kigoma ni asimilima 4.8 ya Tanzania Bara na shughuli
kuu za uchumi ni kilimo, uvuvi na uchakataji wa samaki viwandani.
DC Anga amewaomba wakulima wajenge tabia ya kutumia mbolea kwa ufanisi na hasa
kwa vile Yara imetoa mbolea ya bure kuinua kilimo cha mahindi n mpunga.
Kampuni ya Yara International, imeamua kugawa mbolea bure kiasi cha tani elfu 12 na nusu kwa wakulima wadogo wa Tanzania ili kuimarisha usalama wa chakula katika ngazi ya kaya na taifa kwa jumla. Mbolea iniliyotolewa inakadiriwa kuwa na thamani ya bilioni 16.5/=. Kampuni hiyo imetoa mbolea kwa nchi mbali mbali za Afrika, katika mpango wake unaoitwa Action Africa.
Wilaya Kigoma, inajumuisha sehemu za vijijini na mjini. Kigoma
Vijijini ina watu 489,271 na Manispa ya Kigoma ina watu 144,256.
Serikali inapigana kuinua pato la mwananchi wa kawaida wa Kigoma kutoka
1,152,553/= (makadirio ya 2016) kwa mwaka kwa kutumia kilimo ili
wazalishe mazao yenye soko la ndani na nchi za jirani za Jamhuri ya Watu wa Kongo,
Zambia, Burundi na Rwanda.
Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Mkoa wa Kigoma na asilimia 80 za shughuli
za kiuchumi zinatokana shughuli za kilimo.
Meneja Biashara wa YARA Kanda ya Ziwa, Bw. Phillipo Mwakipesile amewahimiza wakulima kujisajili kwa kupiga *149*46*16#.
"Huu mpango wa kugawa mbolea bure ni dhamira ya kweli ya YARA kuwainua
wakulima wadogo hapa nchini," alisema na kuongeza kuwa hauna uhusiano na
masuala ya siasa.
Comments
Post a Comment