Simbachawene agoma kufungua machinjio ya Msalato iliyochini ya kiwango
Na Jenny Chillery,Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bw. George Simbachawene amegoma kufungua machinjio ya Msalato yaliyopo jijini hapa mara baada ya kubaini mapungufu ya hali ya usafi wa mazingira na ukarabati wa majengo kuwa chini ya viwango.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara katika machinjio hayo, Waziri Simbachawene alisema amefikia uamuzi huo baana ya kubaini mapungufu mengi ikiwemo ukarabati kufanyika chini ya kiwango na pia kutozingatia usafi wa mazingira katika eneo hilo.
“Natoa wiki moja kuhakikisha mkandarasi anafanya marekebisho ya machinjio haya na pia iandaliwe taarifa ya gharama za ukarabati ili tuweze kufanya tathmini ya kilichofanyika na gharama halisi iliyotumika,” alisema Waziri Simbachawene ambaye aliambatana na maofisa kutoka Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Alisema ni muhimu kujiridhisha na kujua gharama iliyotumika kukarabati miundombinu hiyo muhimuna kama vinashabiana na fedha ya watanzania ambayo imetumika katika kazi nzima ya ukarabati.
“Watendaji Serikali ni lazima kuwa makini katika kusimamia miradi ili ifanyike kwa ubora stahiki sambamba na thamani ya fedha zinazotumika ambazo ni za walipa kodi,” alisema na kuongeza kuwa watanzania wana imani na matumaini makubwa na utendaji wa serikali ya Awamu ya Tanochini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliongezea kuwa kilichofanyika katika machinjio hayo kinakinzana na suala zima la utunzaji wa mazingira kwani ujenzi haupo katika mpangilio ambao utayafanya mazingira ya machinjio kuwa katika hali ya usafi na kwa ustawi wa mazngira.
“Sina uhakika kama ujenzi wa machinjio haya umezingatia tathmini ya athari kwa mazingira kwa sababu ujenzi wake haupo katika mpangilio mzuri,” alisema Waziri Simbachawene.
Alisema ziara yake ilikuwa ni kufanya ukaguzi ilikujiridhisha kama ujenzi ulifuata kanuni za mwongozo wa utunzaji wa mazingira kwani ni mwaka moja sasa tangu Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda,Biashara na Mazingira kuifunga machinjio hiyo kwa kuwa haikuwa katika hali salama.
Kwa upande wake Diwani wa eneo hilo la Msalato Bw.Ali Mdende Mohamed alikiri udhaifu uliopo na kuahidi yeye na viongozi wenzake watahakikisha kasoro zote zinarekebishwa kwa wakati.
“Tumejipanga kuhakikisha kasoro zote za ujenzi zinarekebishwa na taarifa ya gharama inapatikana kama alivyoagiza Waziri,” alisema Bw.Mohamed na kuongezea kuwa ukarabati utafanyika ili kuruhusu biashara ziendelee katika machinjio hayo.
Kwa upande wao vijana ambao wanaopata riziki katika machinjio hiyo iliyofungwa kwa baada ya kutishia afya za walaji, wakatoa kilio kwa viongozi kuwajibika, ili machinjio ifunguliwe na wao waendelee kupata kipato.
Bw.Emmanuel Daniel alisema kufungwa kwa machinjio hiyo kumeathiri shughuli za kiuchumi kwani biashara zimesimama kwa muda.
Mchinjaji katika machinjio hayo,Bw.Josephat Chiwanga aliuomba uongozi wa machinjio hayo kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu ilikuondoa sintofahamu zisizo za lazima kwa afya bora watu.
Ziara ya Waziri Simbachawene katika machinjio ya Msalato ni sehemu ya ziara zake za kushtukiza ili kubaini mapungufu na maboresho yanayofanyika katika viwanda na machinjio kwa kuzingatia uhifahdi na utunzaji wa mazingira.
Mwisho
Comments
Post a Comment