Mwekezaji kutoka Misri kujenga kiwanda cha mitungi ya gesi Mkuranga
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Bi. Angellah Kairuki (kulia)
akijadiliana jambo na Mwekezaji na Mwenyekiti wa Kampuni ya Supreme Holding kutoka Misri, Dkt. Moharram Helal
(kushoto) mara baada ya kufanya
mazungumzo kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi huko Mkuranga, mkoani Pwani mwishoni mwa wiki
(katikati) ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya
Intergas, Dkt. Hatem Ahmed ambaye aliambatana
na mwekezaji kwa waziri.
Na Jackson Kulinga. Dar es Salaam
KAMPUNI ya Supreme Holding kutoka Misri inatarajiwa kuwekeza kiasi Dola za Kimarekani Milioni ishirini tano ( zaidi ya bilioni 40) kujenga kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi Wilayani Mkuranga katika Mkoa Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kufanya mazungumzo na mmiliki wa kampuni hiyo, Dkt. Moharram Helal, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Bi. Angellah Kairuki, amesema mbali ya kutengeneza mitungi, kampuni hitakuwa inajaza gesi na kurejeleza mitungi ambayo imeshatumika.
“Hatujawahi kuwa na kiwanda cha aina hii hapa nchini kwani mitungi yote inayotumika kujaza gezi imekuwa ikiingizwa kutoka nje ya nchi. Hii ni fursa ya kipekee kwa Tanzania ambayo ina hazina kubwa ya gesi,” alisema Waziri Kairuki.
Kwa mujibu wa Bi. Kairuki kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kutengeneza mitungi 1,000 kwa siki na pia kujaza gesi kwenye mitungi 3,000 kwa siku ambayo itakuwa na ujazo kati ya kilo 15 na kilo 30.
“Mpaka kiwanda kitapokamilika kitaweza kuajiri watanzania 3,00 na wamisri 30,” alisema na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imeazimia kuifanya Tanzania Kuwa nchi ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025.
Waziri Kairuki amekiagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuhakikisha kinatoa msaada stahiki kwa mwekezaji huyo ikiwemo kujisajili kwa kituo ili awezekunufaika na huduma zinatolewa na kituo kwa wawekezaji hapa nchini.
“Ningependa kuwashauri wawekezaji hapa nchi kuwasiliana moja kwa moja TIC ili kujiepusha na urasimu usio wa lazima kutoka kwa watu wa kati. Nitaendelea pia kuwakumbusha wawekezaji kuendelea kujisajili na TIC kwani faida zake ni kubwa sana,” alisema.
Alisema amemwomba pia Mwekezaji huyo kufikiria pia kuzalisha mitungi yenye ujazo wa chini zaidi ili watu kima cha chini waweze kunufaika na bidhaa zitakazozalishwa au kutengenezwa na kiwanda hicho.
“Tuna mhitaji sana huyu mwekezaji katika eneo hili la kutengeneza mitungi badala ya kuagiza kutoka nje. Nimemwomba afanye mawasiliano na TIC moja kwa moja anapohitaji msaada badala ya kupitia kwa watu wa kati(middlemen).
Bi. Kairuki amemuhakikishia mwekezaji kuwa Tanzania ni sehemu sahihi ya kuwekeza na pia kunafursa nyingi za uwekezaji na mazingira mazuri na rafiki kwa uwekezaji.
Kwa upande wake Dkt. Helal ambaye aliambatana na Meneja Mkuu wa Intergas, Dkt. Hatem Ahmed alimshukuru Waziri Kairuki na kumhakikishia kuwa kiwanda kitakamilika kwa muda mara baada ya kukamilisha taratibu za kisheria.
“Tumeamua kuja kuwekeza hapa Tanzania kwani tuna amini uzoefu tulionao katika kutengeneza mitungi ya gesi utasaidia kufanikisha ujenzi wa kiwanda. Tanzania ni nchi nzuri sana kuwekeza,” alisema.
Mwisho.

Comments
Post a Comment