Simbachawene: Serikali itaendelea kusimamia matumizi ya chuma chakavu
Na Mosses Mahundi, Dar es Salaam
Serikali imesema jana kwamba itaendelea kusimamia kwa karibu sana kuwepo na matumizi ya vyuma chakavu na taka hatarishi kwa
sababu vitu hivyo moja ya rasilimali muhimu sana katika kutekeleza azma
ya serikali ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.
Kauli hii imetolewa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Bw George Simbachawene,
alipotembelea Kiwanda ch OK Plast cha Dar es Salaam ambako ameelezwa kwamba
kiwanda hicho kinatumia chuma chakavu na taka hatarishi kama malighafi ya
kutengeneza nyaya za shaba na kinatumia betri za magari chakavu
kutengeneza mikeke ya kisasa.
Akizungumza na wafanyakazi na viongozi wa kiwanda hicho,
Waziri Simbachawene amesema serikali itaendelea kusimamia kwa karibu marufuku
ya usafirishaji wa chuma chakavu na taka hatarishi ili vitumiwe na
viwanda vya ndani kutengeneza bidhaa kwa soko la ndani na nje.
“Nawashukuru nyinyi OK Plast, kwa sababu mmeonyesha kwa
nini serikali ilifanya maamuzi ya kuzuia usafirishaji wa chuma chakavu na taka
hatarishi nje ya nchi. Viwanda vya ndani ni muhimu sana katika kutoa nafasi za
ajira, lakini pia tutasafirisha bidhaa hizo nje kama ambavyo OK Plast mnafanya.
Hali hiyo itatuingizia pesa za kigeni na kuongeza thamani ya pesa yetu hapa nchini,’’
ameieleza hafla hiyo.
Amesema kuwa ushahidi mwingine wa thamani ya marufuku hiyo ni
kwamba chuma chakavu na taka hatarishi vinavyopatikana nchini bado
vinahitajika mno kwani hivyo vinavyopatikana havitoshelezi mahitaji ya viwanda
vya ndani.
“Duniani kote sasa wanatumia malighafi hizi za vyuma chakavu na
taka hatarishi katika kujipatia malighafi za viwanda vyao. Hivyo nasi hatuna
budi kurejeleza vyuma hivyo ili vitumike kama malighafi katika viwanda vya
ndani,” amewaeleza wafanyakazi na kuongeza kuwa serikali iko makini na
jambo hilo kwa sababu viwanda vya ndani vinachangia ukuaji wa pato la taifa
Akijibu ombi la Afisa Mhakiki wa Kiwanda hicho,
Bw.Anacleto Pereira, kwamba serikali itafute njia nzuri ili kiwanda chao kipate
shaba kutoka kwa wachimbaji wadogo wa shaba nchini, waziri amewashauri
wenye viwanda vinavyotumia shaba katika kutengeneza bidhaa kuweka mipango yao
vizuri ili wanunue shaba kutoka kwa wachimbaji wa ndani.
Bw Pereira ameishukuru serikali kwa kuweka marufuku hiyo na
kueleza kwamba hapo nyuma kiwanda chao na vingine vilikuwa vinakabiliwa na
uhaba wa malighafi hiyo wakati chuma chakavu na taka hatari vinapelekwa nje
kuneemesha watu wengine.
Comments
Post a Comment