Mkuu wa Mkoa Pwani asifu juhudi za mmiliki wa Makampuni ya Global Packaging na Wande Printing
Mkuu wa Mkoa Pwani asifu juhudi za
mmiliki wa Makampuni ya Global Packaging na Wande Printing
Na Abdallah Luambano, Kibaha
Mkuu
wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amemmwagia sifa mmiliki wa Kampuni
ya Global Packaging na Wande Printing and Packaging Ltd, Bw. Joseph Wasonga katika jitihada zake
za kuchangia shughuli za maendeleo
mkoani humo.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika hafla fupi ya makabidhiano ya mifuko 200 ya
saruji kusaidia ujenzi wa ukumbi na ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani
mjini Kibaha, Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Ndikilo amesema kuwa Mwenyekiti wa
Makampuni hayo amekuwa mfano wa kuigwa katika kuchagiza maendeleo katika mkoa
wake.
"Kwa
kipekee kabisa napenda kumshukuru Mwenyekiti wa Makampuni ya Global na Wande
Printing kwa namna anavyojitoa katika kutimiza malengo ya chama na serikali
mkoani hapa jambo linapaswa kuigwa na kila mwekezaji na wadau wote wa
maendeleo,’’ alisema Mhandisi Ndikilo.
Akiongea
kuhusu mchango wa mifuko 200 ya saruji ambayo ilikabidhiwa kwa Ofisi ya CCM Mkoa
wa Pwani, alisema kuwa ujenzi wa ukumbi na ofisi za mkoa utaongeza fursa katika
Mkoa wa Pwani.
“Mchango
huu kwa CCM Mkoa ukitumika vizuri na hatimaye kukamilika kwa ujenzi wa ukumbi
na ofisi utachangia sana kuongeza fursa za ajira, kuongezeka kwa mapato na kuendelea
kuimarika kwa CCM ndani ya Mkoa wa Pwani,’’ alisema Mkuu wa Mkoa.
Aidha,
Bw. Ndikilo alitoa mwito kwa wadau wengine wa chama na serikali kuendelea
kuchangia ujenzi wa ukumbi huo kwani bado upo katika hatua za awali.
‘’Nitoe
wito kwa wadau wa chama kuendelea kuchangia ujenzi wa ofisi hizi kama ambavyo
Katibu Mkuu wa CCM Taifa Bwana Bashiru Ally amekuwa akisisitiza kwamba watu wa
chama waone fahari kuchangia maendeleo ya chama chetu, Bwana Wasonga kaanza na
wengine tufuate,’’ alisisitiza Mhandisi Ndikilo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Global Packaging ambaye alikabidhi mifuko hiyo kwa
niaba ya mwenyekiti wa makampuni hayo, Bw. Benno Mwitumba alisifu Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa Pwani chini ya Mhandisi Ndikilo kwa namna ambavyo imekuwa ikitoa
ushirikiano kwa wawekezaji na wadau wa maendeleo mkoani humo.
‘‘Tunaishukuru
ofisi ya mkoa kwa kutuunga mkono na kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji
hali ambayo imeturahisishia sana katika kuendesha shughuli za uwekezaji katika
viwanda na maeneo mengine ya kijamii,’’ alisema Bw. Mwitumba.
Bw.
Mwitumba alisema kuwa watajitahidi kuongeza ushawishi wao kwa kampuni na
mashirika mbalimbali ya maendeleo ili kufanikisha ujenzi wa ukumbi kwa wakati.
“Taarifa
tulizonazo ni kuwa ukumbi huu unatakiwa kukamilika mwezi wa sita mwakani, kama wadau
wa maendeleo kwa kuungana na CCM mkoa tutakuwa mstari wa mbele katika
kuwatafuta wadau ili waweze kuchangia na kukamilisha ujenzi huu ndani ya muda
uliopangwa,’’ alisema.
Katika
hatua nyingine Bw. Mwitumba alimkabidhi mkuu wa mkoa hundi yenye thamani ya
shilingi milioni moja kama ada ya ushiriki katika maonesho ya viwanda na
kuahidi kutoa mchango wa kuwezesha maonesho hayo yatakayoanza mapema mwezi wa
kumi.
Naye
Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Pwani, Bw. Ally Makoa alimshukuru mmiliki wa
makampuni hayo kwa namna anavyojitoa katika kuijenga Kibaha katika nyanja
mbalimbali na kuwahakikishia kuwa mchango wao utafanya kazi iliyokusudiwa.
Mwisho.
Comments
Post a Comment