SIDO yaibua viwanda 8,477 miaka 5 iliyopita
-->
Na Moses Mahundi, Dar es Salaam
Katika miaka mitano iliyopita
Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limesimamia ujenzi wa jumla ya
viwanda 8,477 ambavyo vimeibua zaidi ya ajira 500,000 jambo limechangia
kukua kwa pato la taifa na kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye uchumi wa kati.
Akizungumza katika mahojiano maalum
kuhusu uhusiano wa dhana ya uchumi wa kati na mchango wa SIDO katika kuifanya
Tanzania kufikia uchumi wa kati jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa
SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji, ameeleza kuwa uchumi wa kati
umefungamana mno na kuwepo kwa viwanda na kwamba SIDO imetekeleza kwa vitendo
sera ya kuanzishwa kwa viwanda ili kufikia lengo la uchumi wa kati.
“Tumepata viwanda vikubwa 201, viwanda
vya kati 460, viwanda vidogo 3406 na viwanda vidogo sana 4410 vimeanzishwa
katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli na
kuliwezesha shirika kufikia asilimia 98 ya malengo yetu,” amesema
Prof.Mpanduji
Viwanda vya ndani hurahisisha na
kuborasha maisha ya watu na kwa kuibua masoko ya malighafi, bidhaa
za viwandani na ajira na hivyo kupunguza umaskini wa kipato.
Prof. Mpanduji amesema soko endelevu na
lenye uhakika ni soko la ndani ya nchi, na kueleza kwamba SIDO
inawahamasisha wazalishaji wa ndani kuzalisha bidhaa zenye ubora ili
Watanzania wapende kununua bidhaa hizo. Amesema ni kwa njia hiyo
Tanzania itawaeza kuimarisha soko la ndani na kulinda viwanda vyake.
“Mteja anapenda kupata bidhaa bora
kulingana na fedha yake. Hivyo ili viwanda ziendelee kuwepo lazima ubora
wa bidhaa uimarishwe ili kujenga imani ya wateja katika soko la ndani na hatua
ya pili ni kuibua fursa ya kupata masoko ya nje ya nchi,” ameeleza.
Amesema ajira nyingi zimezalishwa
na viwanda vidogo sana na viwanda vidogo na kufafanua kuwa sekta ya viwanda
imechangia asilimia 8.5 katika pato la taifa mwaka 2019 na kwamba
mchango huo wa viwanda umehamasisha na kuchochea maendeleo nchini.
“Uwekezaji katika sekta ya viwanda,
hususani viwanda vidogo nchini , umeongeza uzalishaji wa bidhaa mbali mbali
ikiwemo bidhaa za nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, kusindika nyama,
chakula, mboga na matunda, maziwa, mafuta ya kula, sukari, vifungashio, mbolea,
pamoja na viwanda vya kubangua korosho”, amesema Prof.Mpanduji
Ameeleza kuwa katika kipindi cha mlipuko
wa ugonjwa wa Corona, SIDO ilihakikisha viwanda vinazalisha vifaa
vya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo utengenezaji wa barakoa na vifaa vya kujikinga.
“Vita dhidi ya Corona imekuwa rahisi
kutokana na kuwepo kwa viwanda vyenye uwezo ndani ya nchi naupatikanaji
wa bidhaa mbali mbali. Hali hii imepunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje
ya nchi,” alisema Prof.Mpanduji
Prof.Mpanduji amesema kuna ushirikianao
katika ya SIDO na NSSF, VETA, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi(NEEC) na Azania Bank katika kuwawezesha wananchi kupata mafunzo ya
ujasiriamali na mikopo. Mafunzo ni mikopo vitawawezesha wahusika
kuendeleza biashara watakazoanzisha mara baada ya mafunzo.
“Katika ushirikiano huu tunawawezesha
wananchi kupata mikopo kuanzia milioni 5 mpaka milioni 50 na milioni 50 mpaka
milioni 500 kwa Riba ya Asilimia 13, ambapo muda wa mkopo huo ni mwaka 1 mpaka
miaka 7,” alisema Prof.Mpanduji
SIDO inatoa mafunzo ya ujasiriamali na
usimamizi wa biashara katika ofisi zake zilizopo katika kila mkoa nchini lengo
likiwa ni kukuza ujuzi na kujenga ajira nchini.

Comments
Post a Comment