Agricom Tanzania yashinda tuzo zana bora za kilimo
Na Mosses Mahundi, Bariadi
KAMPUNI ya Agricom
Tanzania ambayo inajihusisha na uuzaji pamoja na ushambazaji wa zana za kilimo hapa nchini imeshinda tuzo ya mshindi wa kwanza katika eneo hilo kwenye sherehe za a Nane Nane zilizofanyika kitaifa mkoani Simiyu mwaka huu.
Akizungumzia tuzo hiyo
iliyokabidhiwa na Waziri wa Kilimo,Bwana Japhet Hasunga kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Kaimu Meneja Mkuu wa Agricom, Bw.Remmy Nindi amesema tuzo hiyo imeongeza hamasa kubwa kwa kampuni yake kuendelea kutoa huduma na kushiriki kikamilifu kwenye maonyesho kama hayo kipindi kijacho.
“Tunaishukuru serikali na
waandaaji wa tuzo hizi kwani ni chachu kwetu ya kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma na kuwafikia wadau wengi zaidi katika sekta ya kilimo,” alisema Bw.Nindi.
Alisema zana
mbalimbali za kilimo zilizopelekwa kwenye maonesho mwaka huu ni zenye ubora wa hali ya juu na kukidhi marajio ya wakulima katika ngazi zote ndiyo siri kubwa ya kushinda tuzo.
“Kampuni yetu imekuja
kuziba pengo la uhaba wa zana za kilimo nchini, kwani tumeweza kufungua ofisi katika baadhi ya mikoa na lengo letu ni kuhudumia kanda zote sambamba nakuwafikishia huduma wakulima kwa urahisi zaidi,” alisema Bw.Nindi.
Alisema Agricom Tanzania
ina ofisi maeneo la Melela mkoani Morogoro kwa ajili ya kuhudumia kanda ya mashariki, Kibaigwa mkoani Dodoma kwaajili ya mikoa ya kanda kati, Kahama mkoani Shinyanga kwa mikoa yote ya kanda ya ziwa na Igurusi mkoani Mbeya kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.Aidha, Bw.Nindi alisema maonyesho ya mwaka huu yamekuwa na mwitikio kubwa tangu siku ya kwanza ya ufunguzi kwani wananchi wengi wamekuwa wakijitokeza kutembelea banda la Agricom na kujionea zana mbalimbali za kilimo zinauzwa na kampuni yake.
“Tumeweza kuuza treka, pawatila na majembe. Kulingana na mwitikio wa wakulima wengi tunaimani mashine nyingi zitanunuliwa,” alisema Bw.Nindi na kuongezea kuwa Agricom inatoa pia huduma ya kusambaza zana hizo kote nchini bila kujali mkulima anapatikana mkoa gani.
Katika maonyesho hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipongeza juhudi za Kampuni hiyo katika kuhakikisha zana za kilimo zinapatikana kwa urahisi na wakati hasa katika msimu wa kilimo na kuwezesha mkulima kufanya kilimo cha kisasa.
“Umefika wakati sasa mkulima kuachana na jembe la mkono na kuanza kutumia zana bora za kisasa yakiwemo matrekta na mashine mbalimbali za kuchakata mazao hali itakayosaidia kuongeza tija katika uzalishaji na kuinua kipato cha mkulima ,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aliwataka wakulima nchini kutumia fursa ya mikopo kutoka katika mabenki washirika ikiwemo Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB), CRDB, NMB,NBC pamoja na taasisi nyingine za kifedha ili kuongeza uzalishaji.
Comments
Post a Comment