Zungu ahadi akipa tano kiwanda cha nyaya za umeme
Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano na Mazingira), Mussa
Azzan Zungu(wapili kushoto) akiangilia shughuli zinazofanywa na na Kiwanda cha
Okplast kilichopo Jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya ziara yake kukagua
hali ya utunzaji wa mazingira na pia kusikiliza kero za wawekezaji hao ili
kuzifanyia kazi. katikati ni Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC),Anold Mapinduzi na Kulia ni Afisa
mazingira wa kiwanda hicho,Bw.Gilbert Grid
|
Na Paul Mahundi, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu amekipongeza kiwanda cha
kuzalisha nyaya za umeme cha Ok Plast kwa kufanya uzalishaji unaozingatia
kanuni na taratibu za mazingira na kuahidi kushughulikia changamoto ya uuzwaji
wa taka za mabaki ya shaba nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea kiwanda hicho, Waziri
Zungu alisema kiwanda hicho kinafanya uzalishaji mkubwa wa nyaya za umeme
ambazo soko l;ake kubwa lipo hapa nchini na kuahidi kushughulikia kero ambazo
kiwanda hizo inakumbana nazo.
“Kiwanda kinafanya
uzalishaji mzuri kwa kufuata kanuni na taratibu za mazingira, lakini wamekuwa
na changamoto ya utunzaji wa taka baada ya kuyeyushwa kwa shaba ambayo kwa hapa
nchini hazina soko. Nitaagiza timu ya wataalamu kuja kuangalia madhara
yanayoweza kupatikana kwa kusafirishwa taka hizo nje ya nchi kabla ya kutoa
kibali,’’ alisema Waziri Zungu.
Waziri alisema licha ya
kushughulikia changamoto ya kiwanda hicho, amewataka wenye viwanda kote nchini
kuacha kuhujumu miundombinu ya umeme, maji na madaraja kwa lengo la kupata
malighafi za kuzalishia nyaya za umeme.
“Serikali ya awamu ya tano
inatekeleza seraya uchumi wa viwanda. Utekelezaji wa azma hiyo lazima uende
sambamba na utunzaji wa miudombinu yetu ya madaraja, umeme na maji. Natoa wito
kwa wenye viwanda kuacha kuhujumu miundombinu ambayo serikali imetumia pesa
nyingi za walipa kodi wa Tanzania kuijenga,’’ alisema.
Katika hatua nyingine
amewataka wenye viwanda kuweka miundombinu rafiki katika kuhakikisha wanazuia
kusambaa kwa hewa chafu ambayo imekuwa inazalishwa viwandani na hivyo kuleta
athari kubwa kwa wakazi wa maeneo kuzunguka viwanda na pia kusababisha
mabadiliko ya tabia nchi.
“Viwanda lazima vikidhi
vigezo vya mazingira ikiwemo kutibu maji kabla ya kutitirishwa na namna nzuri
ya kudhibiti hewa yenye ukaakaa ambayo imekuwa na athari hasi kwa viumbe hai
pamoja na kusababishwa kwa mabadiliko ya tabia nchi,’’ alisema na kuongeza kuwa
Wizara yake haitawavumilia wawekezaji wa aina hiyo.
Kwa upande wake Afisa
Mazingira wa kiwanda hicho, Bw. Gilbert Grid licha ya kupongeza ujio wa Waziri
kiwandani hapo, alisema kiwanda chao kitaendelea kufanya uzalishaji kwa kufuata
kanuni na taratibu zote za mazingira ili kujiepusha na migongano na taasisi za
serikali ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
”Kumekuwa na ufuatiliaji wa
muda mrefu wa namna ya kusafirisha mabaki ya shaba (slime & slug) nje ya
nchi ambako soko lipo, ujio wa Waziri ambaye amejionea uzalishaji na uwepo wa
mabaki hayo ni hatua muhimu kwa kiwanda kwa kuwa yanapobaki hapa kiwandani
tunakosa nafasi lakini pia tunakosa mapato kwa kuwa huko nje yanahitajika,’’
alisema Bw. Grid bila kutaja nchi zinazohitaji taka hizo.
Naye Meneja wa NEMC Kanda
ya Mashariki, Arnold Mapinduzi amewataka wenye viwanda wanaotumia malighafi za
vyuma chakavu kufuata taratibu ikiwemo kununua malighafi hizo kutoka kwa wenye
vibali vya ukusanyaji na usafirishaji.
“Waziri ameelekeza mambo ya
kufanya kwa upande wa kanda ya mashariki, lakini pamoja na hayo, tunawataka
wenye viwanda kununua vyuma chakavu kutoka kwa wakusanyaji wenye vibali.
Kutokujua Sheria haitokuwa kama kisingizio kwa yeyote atakayebaini kukiuka
utaratibu huo,’’ alise Bw. Mapinduzi.
Comments
Post a Comment