Sima aagiza waliojenga katika msitu wa Slender wachukuliwe hatua mara moja
Na Abdallah Luambano, Dar es Salaam
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
Mussa Sima ameghadhabishwa na ujenzi wa nyumba katika eneo la Msitu
wa asili wa Slender alilolitembelea jana Jijini Dar es Salaam na
kuiliagiaza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC)
liwachukulie hatua watu ambao wamejenga na kufanya shughuli nyingine za
kibinadamu katika eneo hilo.
Waziri ametembelea eneo la mikoko kando ya daraja la
Slender baada ya kuwepo taarifa za kuendelea kwa shughuli za kibinadamu katika
msitu huo wa asili ikiwemo ujenzi wa nyumba na utiririshaji wa maji
taka baharini, wakati serikali inajenga daraja refu la kisasa ili kulifanya
Jiji la Dar es Salaam liwe na mvuto wa kimataifa.
“Eneo la Slender ni miongoni mwa maeneo ya kimkakati katika utunzaji
wa mazingira kama yalivyo maeneo mengine kote nchini yenye uoto wa asili. Eneo
hili lipo ndani ya hifadhi ya mazingira na serikali haitakubali kuona shughuli
zozote za kibinadamu zikiendelea katika eneo hili pamoja na maeneo mengine
muhimu kote nchini,’’ amesisitiza Waziri Sima.
Bw. Sima ameitaka NEMC) kufuatilia kwa karibu watu wote ambao
wamefanya shughuli za kibinadamu katika eneo hilo na kuwachukulia hatua za
kisheria.
“Kumekuwepo na shughuli za kibinadamu katika eneo hili ikiwemo
ujenzi na utiririshaji wa maji taka ambayo yanaingia baharini na kuleta madhara
kwa viumbe wanaoishi majini. Naliagiza Baraza kuwatafuta watu wote ambao
wamekuwa wakifanya shughuli hizo na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,’’
amesema.
Bw. Sima ametoa wito kwa Watanzania kutunza mazingira ikiwemo
maeneo maalumu ambayo yametengwa na serikali kama sehemu ya maeneo ya uoto wa
asili.
“Yanayofanyika hapa ndiyo yanayofanyika katika maeneo mengi
yaliyotengwa na serikali hapa nchini. Tumejipanga kuyalinda mazingira na yeyote
atakayebainika kuyaharibu sheria itachukua mkondo wake,’’ alisema.
Mkurugenzi wa Sheria wa NEMC Benard
Kongola, ameeleza kuwa eneo hilo limekuwa na mgogoro kwa muda mrefu
kidogo na kwamba baraza limekuwa likichukua hatua kuhakikisha hakuna shughuli
zozote zinafanyika katika eneo hilo.
“Pamoja na maagizo ya Waziri ambayo tutayafanyia kazi mara moja,
tunapendea ieleweke kwamba Baraza limekwishawaripoti watumishi wa Baraza ambao
walishikiriana na wanufaika wa eneo hili kughushi nyaraka za kurasimisha eneo
hilo kwa shughuli za kibinadamu,’’ ameeleza Bw. Kongola.
Amesema NEMC pia wamekuwa wakitembelea eneo hilo mara kwa mara
kukagua mazingira ya eneo hilo na kuchukua hatua ikiwemo kuwapiga faini
wanaotiririsha maji machafu baharini.
Amesema mbali ya kuwapiga faini wakazi waliobainika
kutiririsha maji katika msitu huo, NEMC imewaelimisha njia nzuri za
kutumia kulinda mazingira ili maji machafu yasiingie
baharini na kuathiri viumbe vya baharini.
Baraza linachukua hatua za kimkakati kulinda mazingira na
kuungamkono azma ya serikali ya ujenzi wa viwanda.
Comments
Post a Comment