Chuo cha diplomsia kutumia bilioni 12 kujipanua-Dkt Ponera
Na Abdallah Luambano, Dar es Salaam
CHUO cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR) cha Jijini Dar es Salaam kinarajia kutumia kiasi cha jumla ya shilingi bilioni 12 za kitanzania kwaajili ya kujipanua ikiwemo ujenzi wa majengo mapya na kuanzisha kampasi mpya mikoani ili kuongeza idadi wanufaika wa programu na kozi zinazotolewa na chuo hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Chuo hiyo, Dkt. Jeremia Ponera amesema kujipanua kwa chuo kunakwenda sambamba na kuongeza programu na kozi mbalimbali ili kukidhi matakwa na mahitaji ya soko la ajira hapa nchini.
“Tunapenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutenga fedha kwaajili ya upanuzi wa chuo hiki. Tutajenga vyumba vya mihadhara, maabara ya lugha, maktaba ya kisasa, vyumba vidogo vya kufundishia na semina, hosteli za wanafunzi pamoja na maeneo ya kujifunzia,” alisema Dkt. Ponera.
Dkt. Ponera alisema mradi wa upanuzi wa chuo utasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 1,500 hadi kupifikia wanafunzi 4,000 kwa Dar es Salaam peke yake.
“Tunarajia kufungua kampasi tatu Dodoma, Arusha na Zanzibar ilikupanua wigo na kutoa fursa kwa watanzania wengi wenye kiu ya kujiunga na programu pamoja na kozi mbalimbali waweze kufikiwa kwa haraka,”alisema.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo elimu inayotolewa na CFR itakuwa imewafikia watanzania wengi mikoani ambao walikuwa wanalazimika kuja Dar es Salaam kwaajili ya kujiunga na programu na kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo.
“Tumeshafika Dodoma na tupo katika hatua za mwisho za kupata ardhi na kuanza ujenzi na tunategemea katika kipindi cha miaka mitatu ijayo tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa kampasi yako,” alisema Dkt. Ponera na kuongeza kuwa Chuo kimeshapata pia kiwanja katika mkoa wa Arusha. Alisema CFR kimejipanga kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Uchumi wa Kati na Viwanda ifikapo mwaka 2025, sambamba na kujenga ufahamu, kuvutia uwekezaji na biashara za kimataifa.
“Chuo cha Diplomasia kinaandaa na kutoa mafunzo kutokana na uhitaji mbalimbali katika jamii,” alisema na kuongeza pia chuo chake ni hazina kubwa ya maarifa katika nyanja za diplomasia na uhusiano wa kimataifa.
Kwa upande wake,
Mrajisi (Registrar) wa Chuo hicho, Dkt.ally Masabo alisema chuo kwa sasa
kinatoa program za Astashada, Stashada, Shahada na Shahada za Uzamili katika
nyanja mbalimbali.
“Tunazo pia kozi fupi fupi ambazo mtu yeyote anaweza kujiunga kwani hazihitaji sifa za kujiunga. Tunawakaribisha watanzania kuja kutembelea na kujifunza kozi mbalimbali ilikujiongezea maarifa,” alisema Dkt. Masabo.
Kituo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa kilianzishwa mwaka 1978 kwa ubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Msumbiji. Kimepewa jukumu la kuwaandaa watanzania katika mafunzo ya diplomasia, lugha,stratejia na diplomasia za kiuchumi.
Comments
Post a Comment