Msimwage majitaka katika mitaro ya mvua, NEMC yaonya wakazi wa mijini


Na Mosses Fedirnand, Dar es Salaam
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka Watanzania,hasa waishio mijini,  kuacha kabisa kutiririsha majitaka katika mitaro iliyojengwa kusafirisha maji ya mvua kwani tabia hiyo inahatarisha afya ya umma na kuharibu mazingira.
Akiongea jana baada ya kutembelea eneo la makazi la Mabibo na Ukanda Maalumu wa Viwanda katika eneo hilo, Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka, amesema ameshtushwa kuona wananchi wameelekeza mabomba ya majitaka kutoka majumbani mwao na  kumwaga majitaka  hayo  katika mtaro mkubwa wa umma unaosafirisha maji ya mvua hadi Mto Msimbazi na kwenda baharini.   NEMC imekuwa ikikemea tabia hiyo mara kwa mara.
Amesema jambo hilo limemsikitisha sana na kufafanua kwamba  kasoro hiyo inahatarisha afya ya wananchi wa Mabibo na wa mbali  na kuharibu mazingira.  “Wananchi kuelekeza mabomba ya majitaka kwenye mitaro maalumu ya umma siyo matumizi sahihi ya mitaro hiyo ya umma.  

Tunawaonya wananchi wanaofanya hivyo nchini kuacha mara moja tabia hiyo kwani inahatarisha afya ya umma na kuaharibu mazingira,” ameeleza. Dk Gwamaka ametembelea eneo la Mabibo baada ya NEMC kupokea barua inayolalamikia kiwanda cha kutengeneza nguo kwa uchafuzi wa mazingira kwa njia ya moshi, kelele na maji yenye kemikali na sumu.   “Jambo hili litafuatiliwa kwa makini kwa kuunda timu ya wataalaamu.  Ikibainika kwamba kiwanda chochote kimekiuka matakwa ya Sheria ya Mazingira ya 2004, hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” ameeleza.
Hata hivyo Dk Gwamaka amewataka wananchi  kuacha tabia ya kunyoshea vidole taasisi au kiwanda huku wao wakiwa mstari wa mbele  katika kuharibu mazingira badala ya kuyalinda.
Mtaalamu huyo amewataka wananchi na viongozi  kuelewa kwamba mazingira salama ni muhimu kwa ustawi wa watu, wanyama na viumbe vingine na kuwaomba viongozi wa serikali za mitaa kuhakikisha miundombinu inatumika kwa shughuli tu liliyokusudiwa.  “Mamlaka zote tukisimamia hili tutaepusha madhara kwa wananchi, mifugo na viumbe vingine vilivyomo katika mazingira yetu,”ameeleza.

Dr Gwamaka amewataka Watanzania kuyalinda mazingira wakielewa kwamba ustawi wa wao  na shughuli nyingine zote zinategea usalama wa mazingira ya Tanzania.  Hakusema ni lini timu ya wataalamu itaanza kazi yake lakini amedokeza kuwa timu itaanza kazi yake baada ya muda mfupi ujao.

Comments

Popular posts from this blog

Tanzania praised for being keen on fertilisers going to farmers

Gold mine in Songwe wins ministerial praise for protecting environment

NEMC warns on emptying effluent in built-up areas, flood waters