Wajasiriamali wanawake waelezwa fursa zilizopo Comoro



Na Daniel Lwimiko, Dar es Salaam

NAIBU Balozi wa Comoro nchini Tanzania,  Balozi Bacar Salim,
ameuambia mkutano  wa maandilizi ya Maonyesho ya Bidhaa za Tanzania
yanayotarajiwa kufanyika Comoro katikati  ya mwezi kesho kwamba
washiriki wapeleke Comoro  bidhaa za chakula, viungo, dawa za asili,
asali, dagaa pamoja na bidhaa za viwandani, hasa samani za ndani.

Mkutano huo umeitishwa na Mfuko wa Saccos wa Wajasiriamali Tanzania
(TASWE) au Tanzania Saccos for Women Entrepreneurs kuwaandaa
wajasiriamali watakoshiriki katika maonyesho ya siku nane
yanayotaratijiwa kufunguliwa na Rais wa Comoro, Aprili  17 na kufungwa
Aprili 24, mwaka huu.  Maonyesho hayo yatavuma kama Wajasiriamali
Wanawake wa Tanzania Tumekuja Comoro.

“Jambo muhimu kwenu ni kujua bidhaa ambazo Wakomoro wanazihitaji. Kwa
muda mrefu tumekuwa tukiagiza bidhaa za chakula, viungo, dawa za
asili, asali, dagaa pamoja na bidhaa za viwandani kutoka nchi
mbalimbali. Hivyo wakati mkijiandaa na ziara hiyo ya kibiashara  ni
vyema mkaangalia hayo maeneo,’’ ameshauri  Balozi Salim.

Naibu balozi huyo amepongeza jitihada  za akina mama ambazo amesema
zinaimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Comoro.

Amesema watu  wa nchi hizo mbili  wamekuwa wakifanyabiashara kwa muda
mrefu.  “Hivyo ni jukumu letu kuweka mazingira mazuri na ambayo ni
endelevu kwa manufaa ya vizazi vya leo na kesho.’’
 Mwenyekiti wa TASWE, Bi Anna J. Matinde amesema kuwa maandalizi yote
ya safari hiyo yamekamilika.

“Kwa kiasi kikubwa maandalizi ya safari yamekamilika. Kwa sasa
tunaangalia mambo machache ikiwemo viza. Makadirio yetu yalikuwa
tuondoke na wajumbe 60 lakini mkutano huu umeongeza hamasa kwani
wajumbe wengine wamejitokeza na hivyo kuongeza idadi ya washiriki,’’
ameeleza Bi Matinde, na kuwapongeza  wajumbe kwa kuhudhuria mkutano
huo  ambao amesema umewapa  nafasi ya kufahamu  fursa za biashara
zilizopo nchini Comoro.

“Tumekuwa tunapata shida kueleza  fursa zinazopatikana nje ya mipaka
yetu.  Lakini kuwepo kwa ujumbe mzito kutoka Ubalozi wa Comoro hapa
nchini kumerahisisha kufikisha ujumbe na Watanzania wamesikia.
Tunaamini kuwa maonyesho haya yatakuwa ya mafanikio makubwa,’’
alisema.

Meneja wa TASWE, Bi Lilian Nyagabona,  ambaye anasimamia iitifaki,
ameeleza kuwa maonyesho hayo yanayotarajiwa kufunguliwa na Rais wa
Comoro. “Haya yatakuwa ni maonyesho yenye mvuto wa aina yake kwani
serikali za nchi zote mbili wameyabariki na tutaondoka hapa.  Taarifa
tulizonazo ni kwamba yatahudhuriwa na watu wengi wakiwemo
wafanyabiashara na wakezaji wa huko Comoro,’’ ameeleza Bi. Nyagabona.
Mwisho.

ReplyReply allForward



Comments

Popular posts from this blog

Mbeya agro-processors get 5 acres to build 50 industries

Tanzania praised for being keen on fertilisers going to farmers

Gold mine in Songwe wins ministerial praise for protecting environment