Kampuni ya Agricom Africa yamkuna RC Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Bw. Loatha Sanare
ameridhishwa na kupongeza
kazi zinazofanywa na kampuni ya
Agricom Africa mkoani mwake kwani zinatafsiri
kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga ujenzi wa uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.
Mkuu wa Mkoa huyo amesema katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Bw. Mohamed Utaly katika hafla ya kuhitimu mafunzo ya wiki sita yalitolewa na Agricom Africa kwa vijana juu ya uendeshaji na utengenezaji wa zana za kisasa za kilimo yakiwemo matrekta na pawatila.
“Natumia fursa hii kuishuru kampuni hii ya Agricom Africa kwa kazi kubwa inayofanya katika Mkoa wa Morogoro na hasa kuandaa mafunzo haya kwa vijana kwani yatasaidia kuchochea ukuaji wa teknolojia katika kilimo,’’ alisema.
Bw. Sanare alisema uwekezaji katika sekta ya kilimo lazima utiliwe mkazo hasa katika kipindi hiki ambacho serikali imeazimia kuleta mageuzi ya uchumi wa kati na viwanda kwa sekta ya kilimo ndiyo mchagizaji mkubwa katika kufanikisha azma hiyo.
“Hakuna maendeleo ya viwanda kama sekta ya kilimo haitafanya mageuzi makubwa, hivyo wakati serikali ikiwa imejikita na azma ya ujenzi wa viwanda ifikapo 2025, lazima kuhamasisha wadau wa kilimo na maendeleo kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta hii ili kupata malighafi ya kutosha ambazo zitatumika katika viwanda vyetu,” alieleza Bw. Sanare.
Aidha Bw. Sanare alitoa wito kwa wahitimu hao kutumia vyema mafunzo waliyoyapata ili waweze kujinufaisha kiuchumi na kuchangia mageuzi katika kilimo hali ambayo itaongeza pato la nchi.
“Kilimo ni sekta ambayo imeajiri zaidi ya asilimia 65 ya watanzania na kuchangia asilimia 28 katika pato la Taifa. Mkatumie ujuzi mliopata ili kujipatia ajira na kuongeza chachu katika ukuaji wa sekta hii,’’ alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamapuni hiyo Bi. Angelina Ngalula aliishukuru serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji licha ya mkoa huo kukabiliwa na migogoro mingi ya wakulima na wafugaji huko nyuma.
“Miaka kadhaa iliyopita ilitawaliwa na migogoro ya wakulima na wafugaji, hali hiyo haikuwa rafiki kwa wawekezaji, lakini serikali ya mkoa ilipambana na sasa Morogoro hali ni shwari na imetuvutia kuja kuwekeza,’’ alisema Bi. Ngalula.
Bi. Ngalula pia ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) aliishukuru pia Mamlaka ya Elimu nchini (TEA) ambayo imepewa jukumu la kusimamia miradi ya ujuzi hapa nchini kuendelea kutoa pesa ili kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali.
“Kwa namna ya kipekee kabisa tunawashukuru wenzetu wa TEA ambao walikuwa wadhamini wa mafunzo haya yaliyolenga kuwapa vijana ujuzi. Tunaomba msituchoke kwa wakati mwingine tutakapowafuata ili kuendelea na jukumu la kuwapa ujuzi vijana wa kitanzania,’’ alisema Bi Ngalula.
Alisema ni ndoto kwani hakuna mtu yeyote kutoka nje ya nchi atakayeifanya Tanzania kufikia azma ya uchumi wa kati na viwanda zaidi ya kuunganisha nguvu zetu kutoka sekta binafsi na za umma.”
Naye, Bw Ally Baraka miongoni mwa wahitimu 135 wa mafunzo hayo alisema wataitumia vyema elimu waliyoipata kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo.
Mafunzo hayo ya wiki sita yaliandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na Agricom Africa na kudhaminiwa na TEA ili kuwapa vijana ujuzi katika sekta ya kilimo.
Comments
Post a Comment