NEMC yakunjua makucha, yakitoza faini kiwanda cha kuzalisha mifuko mbadala.
Na Isdory Njavike Dar es salaam
Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
limekipiga faini ya shilingi milioni 35 kiwanda Cha kuzalisha mifuko mbadala
cha Al-Haseeb Jewellery Limited kwa makosa mbalimbali likiwemo la kuzalisha
mifuko mbadala iliyo chini ya kiwango cha 70gsm.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya siku moja
katika kiwanda hicho kilichopo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa NEMC
Dkt. Samuel Gwamaka akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Ngenya Athuman alisema uzalishaji wa mifuko mbadala
iliyo chini ya kiwango imekua changamoto kubwa kwa Baraza pamoja na
wafanyabiashara wa mifuko hiyo wanaofuata sheria na taratibu zilizopo.
Alisema viwanda kama cha Al-Haseeb Jewellery ni moja ya vikwazo
vinavyorudisha nyuma juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kutekeleza
azma ya Serikali ya ujenzi wa viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.
"Tumepata malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara
wanaofuata sheria kuwa sokoni mifuko yenye kiwango cha 70gsm haiuziki, na
tulipofanya uchunguzi tukagundua uwepo wa wazalishaji kama hawa ambao wamejaza
sokoni mifuko isiyokidhi vigezo, huu ni uhujumu wa uchumi kwa taifa,” alisema
Bw. Gwamaka.
Dkt. Gwamaka aliyataja makosa ambayo kiwanda hicho inakabiliana
nayo kuwa ni pamoja na kuzalisha mifuko mbadala zaidi ya milioni mbili
iliyochini ya kiwango na kupigwa faini ya milioni 20, kufanya uzalishaji bila
kufanya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) ambapo faini yake ni milioni 10
pamoja na milioni 5 kwa kusambaza mifuko hiyo katika masoko mbalimbali.
"Fuateni sheria zilizopo kinyume na hapo madhara yake ni
makubwa. Ninawaonya wamiliki wengine wa viwanda visivyofuata sheria kufuata
sheria kwani mpango wa NEMC ni kuwabaini wote wanaoendesha viwanda kinyume na
utaratibu. Nia yetu ni kulinda viwanda vya ndani vinavyofuata sheria ili kuweza
kutimizia azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa nchi ya uchumi wa Kati na
viwanda ifikapo mwaka 2025," Dkt. Gwamaka alisisitiza
Hata hivyo Dkt. Gwamaka aliongeza kuwa tayari Kuna baadhi ya
wafanyabiashara wanaouza mifuko hiyo chini ya kiwango wameshakamatwa na
watafunguliwa mashtaka. Aliomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa
kuripoti mambo yote yanayohusiana na uvunjifu wa sheria ya Mazingira na wao
watafanyia kazi taarifa hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa (TBS) Dkt. Athuman
amesema shirika lake halitakuwa na huruma dhidi ya wenye viwanda ambao wamekuwa
wakizalisha bidhaa zao chini ya kiwango na wataendelea kuchukua hatua za
kisheria.
"Hatuwezi kuchekea vitendo Kama hivi vinavyorudisha juhudi
za rais wa nchi yetu, tumejipanga vizuri na tutapambana na kila mtu anaekiuka
taratibu zilizopo atashughulikiwa kwa mujibu wa sharia,” alisema Dkt. Athuman.
Comments
Post a Comment