Benki ya Kilimo yakabidhi matrekta Zanzibar

Benki ya Kilimo yakabidhi matrekta Zanzibar
Na Mwandishi Wetu, Unguja

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo nchini(TADB) itaendelea kushirikiana na
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar kutoa elimu kwa
wakulima kuhusu umuhimu wa Mikopo inayotolewa benki hiyo ili kuongeza
uzalishaji wenye tija na kuinua maisha ya mkulima.

Akizungumza mara baada ya kumkabidhi matreka mawili yenye thamani ya
zaidi ya shilingi za kitanzania milioni 150 Rais wa Zanzibar Dkt Ali
Mohammed Shein,  Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji  wa TADB, Bw.Derick
Rugemala alisema matreka yatagaiwa kwenye vyama vya msingi vya
wakulima.

“Tumekabidhi matreka haya yaweze kusaidia sekta ya kilimo na kuongeza
uzalishaji wa mazao hasa mpunga hali itakayosaidia kuongezeka kwa
kipato cha mkulima,” alisema Bw.Rugemala na kuongeza kuwa zoezi hilo
limefanyika sambamba na ufunguzi wa sherehe za Nanenane.

Alisema TADB itaendelea kushirikiana pia na wakulima ndani ya Zanzibar
 ili waweze kunufaika na uwepo wa benki ya kilimo ambayo ndiyo
mkombozi katika kutatua changamoto za wakulima nchini.

“Lengo la TADB ni kuona tija katika uzalishaji wa mazao nchini
unaongezeka na kwa kuhakikisha hilo linafanikiwa benki inaendelea
kuhamasisha wananchi kutumia fursa ya uwepo wa benki hiyo katika
kupata mikopo itakayosaidia kukuza shughuli za kilimo,” alisema
Bw.Rugemala.

Aliongezea kuwa Benki inawawezesha wananchi kwa kuwapatia  mbinu na
elimu ya kilimo cha kisasa na pia mitaji katika kuendeleza sekta ya
kilimo lengo likiwa kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa
kati na viwanda.

“Mkakati wa TADB ni kuongeza uzalishaji katika mnyororo wa thamani
katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi hivyo tunahakikisha mazingira
yanakuwa wezeshe katika uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao na
kuyafikia masoko,” alisema Bw.Rugemala.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakulima waliotembelea banda la TADB
katika maonesho ya kilimo Zanzibar waliishukuru benki hiyo kwa  kutoa
matreka ambayo yatawasaidia katika kuendeleza kilimo.

Mkulima, Bw.Juma Hajji alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo
katika kilimo ni nyenzo za kilimo hivyo kupatikana matrekta haya
yatasaidia  kilimo kuwa cha kisasa na kuongeza  tija na  uzalishaji wa
mazao..

“Kwa kuletewa treka hizi wakulima tunauhakika sasa wa kuongeza
uzalishaji wa mpunga na hatimaye kujitosheleza kwa chakula na hata
kufikia kuuza katika masoko ya nje,” alisema Bw.Hajji.
Afisa kutoka Wizara ya Kilimo, Maliasili, mifugo na Uvuvi Nassor Salim
Mohamed alisema utaratibu mzuri utawekwa wa namna bora ya matumizi ya
matrekta ili wakulima wengi waweze kunufaika.

Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

Mbeya agro-processors get 5 acres to build 50 industries

Tanzania praised for being keen on fertilisers going to farmers

Mavunde: TADB offered 1.8bn/- to nurture Farm Access