TADB, NFRA wawahakikishia wakulima soko la mahindi

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula(NFRA) Bi.Vumilia Zikankuba(kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) Bw.Japhet Justine mara baada ya kumaliza kikao kilicholenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa mahindi ili kuleta tija na kuwawezesha wakulima wadogo wadogo wa zao hilo hapa nchini kwa kuwapatia soko la uhakika la mazao yao.

Na Moses Ferdinand, Dar es salaam

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) kwa kushirikiana na Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula(NFRA)  wameingia makubaliano kuongeza thamani ya mnyororo wa thamani wa zao la mahindi kwa kuhakikisha wakulima wa zao hilo hapa nchini wanapata soko la uhakika  ili waweze kunufaika na shughuli ya kilimo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kikao cha pamoja, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine alisema wamekubaliana na NFRA kuhakikisha zao la mahindi linapata soko jambo litakalompa uhakika mkulima kuendelea na kilimo cha zao hilo.

“TADB ilishatoa zaidi ya bilioni 3.4 kwa vikundi 22 vya wakulima katika kufanya kilimo cha kisasa cha zao la mahindi, hivyo kupitia kikao hiki  tunawahakikishia wakulima wa mahindi soko la uhakika,” alisema Bw.Justine

Alisema kwa msimu wa kilimo uliopita soko la zao la mahindi liliyumba hivyo kupitia mazungumzo kati ya TADB na NFRA yataibua matumaini kwa wakulima wengi wa mahindi kwa kupata soko la bidhaa hiyo ambayo bei yake ilishuka kutokana na uzalishaji kuongezeka tofauti na mahitaji ya nchi.
“Pamoja na Shirika la Chakula Duniani(WFP) kununua zaidi ya tani 36,000 za mahindi bado shehena nyingi za mahindi zipo kwa wakulima, hivyo kama wadau wa sekta ya kilimo ni wajibu wetu kuhakikisha shehena hizo zinapata soko,” alisema .

Hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli alishuhudia utiliaji wa makubaliano Ikulu Jijini Dar es Salaam kati Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na WFP kuhusu kununua kiwango kikubwa cha mahindi.

Bw.Justine alisisitiza kuwa ili kumfanya mkulima kuendelea na kilimo cha zao hilo ni lazima ahahakikishiwe soko la bidhaa yake itakayompa hamasa ya kulima kwa tija ili aweze kupata mavuno kwa wingi na tija inayotakiwa sokoni.

“TADB itaanda mkakati wa pamoja na NFRA utakaoleta mabadiliko makubwa katika mnyororo wa thamanai wa zao la mahindi nchini, hii ni kutokana ana changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika msimu wa kilimo uliopita ulifanya zao la mahindi kushuka thamani,” alisema Bw.Justine

Aliongezea kuwa kupitia mikataba wanayoingia NFRA na wanunuzi kutoka nje ya nchi itatupa mwongozo wa kuhamasisha kilimo nchini kwa kuwakopesha wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima wadogo(SCGS) katika kufanya kilimo chenye tija na kukidhi mahitaji ya soko.

Alisema lengo letu ni kuhakikisha bei ya zao hili sokoni inakuwa ya kumnufaisha mkulima kwa kipindi chote cha msimu hali itakayomfanya mkulima kurudisha fedha yake na kupata faida itakayompelekea kufanya maendeleo.

“Serikali ya Awamu ya Tano Chini ya Rais Dkt.John Magufuli imejipambanua kuboresha mazingira ya wananchi wa hali ya chini wakiwemo wakulima, hivyo TADB kwa nafasi yetu tunaendelea kutekeleza azma ya Serikali kwa kuboresha mazingira kwa wakulima nchini,” alisema Bw.Justine

kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA Bi.Vumilia Zikankuba alisema wamefanya mazungumzo mazuri na TADB ambayo yatawasaidia kama wakala katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha zao la mahindi linapata soko.

“NFRA imejipanga kupunguza utegemezi kwa Serikali katika kufanya shughuli zake, hivyo tunashirikiana na wadau wa kilimo na Taasisi za kifedha kama TADB kutuwezesha fedha zitakazo tusaidia kuendesha shughuli zetu za uhifadhi wa mazao na kujenga masoko,” alisema Bi.Zikankuba

Alisema kupitia mazungumzo yetu tunauhakika wa kupata fedha zitakazo kuwezesha kununua mahindi kutoka kwa wakulima hivyo kutoa uhakika kwa mkulima kuwa soko la zao hili lipo na kama wakala tutajitahidi kuhakikisha tatizo la ukosefu wa soko unapungua au kuisha kabisa.

Wakulima wa Mikoa ya Nyanda za juu Kusini ikiwemo Ruvuma,Rukwa wamekuwa wakilalamikia soko la mahindi hivyo kuiomba Serikali kuisaidia kupata soko la uhakika kwa ajili ya zao hilo ili kuweza kumudu bei  za pembejeo za kilimo.

Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

Mbeya agro-processors get 5 acres to build 50 industries

Tanzania praised for being keen on fertilisers going to farmers

Mavunde: TADB offered 1.8bn/- to nurture Farm Access