Bashungwa avutiwa na kazi za SAGCOT


Naibu Waziri wa Kilimo Innocent Bashungwa (kushoto) akizungumza jambo alipotembelea makao makuu ya ofisi za Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) mara baada ya kupewa maelezo juu ya utendaji kati wa kituo hichi katika kuinua sekta ya kilimo nchini. kulia niAfisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho,Bw.Geoffrey Kirenga


Na Jackson Kulinga, Dar es salaam

NAIBU Waziri wa Kilimo, Bw. Innocent Bashungwa amepongeza kazi inayofanywa na Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini(SAGCOT) kwa kuweza kuwafikia wakulima wengi katika ukanda huo na kufanya mageuzi kwenye sekta ya kilimo kwa kuongeza tija katika uzalishaji.

Akizungumza katika ziara yake ya kwanza  alipotembelea  Kituo hicho jijini Dar es salaam  mwishoni mwa wiki ilikujionea utendaji kazi wake, naibu waziri Bashungwa alisema amefurahishwa na kazi zinazofanywa na  kituo hicho ikiwemo kuwaunganisha wakulima na kuwajengea uwezo na mbinu za kilimo biashara.

“Ziara yangu katika ofisi yenu imekuja mara baada ya kuona kazi nzuri na ushuhuda mbalimbali kutoka kwa wakulima katika mikoa ya Njombe na Iringa hivyo ikanisukuma  niwatembelee  ili tufahamiane na kujifunza kazi zenu,” alisemaBw. Bashungwa.

Alisema utendaji kazi wa SAGCOT umeleta matokeo chanya kwa wakulima katika mikoa ya nyanda za juu kusini hivyo ni muhimu kwa wadau mbalimbali wa kilimo kote nchini kujifunza kupitia mfumo unaotumiwa na SAGCOT ili  kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo.

“Uzalishaji umeogezeka katika maeneo ambayo SAGCOT inafanya kazi na wakulima. Hii imepelekea uchumi kwa wakulima kuimarika kutokana na uhakika wa uzalishaji na masoko ambapo SAGCOT ndiyo muunganishi,” alisema.

Alisema  kwa kufuata mfumo huu wa SAGCOT,  utekelezaji wa Mpango wa Awamu ya  Pili wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP  II) utakuwa wa mafanikio kwani njia nzuri imeonyeshwa kupitima maeneo ambayoyo SAGCOT inafanya kazi zake.

“Wakulima wa chai mkoani Njombe wamefaidia kwa kilimo cha chai kupitia washirika wa SAGCOT ambao ni Kampuni ya kuhudumia wakulima wadogo Njombe(NOSC), hii inaonesha ni kwa namna gani SAGCOT imejipanga kuleta mapinduzi ya kilimo nchini,” alisema Naibu Waziri Bashungwa.

Aidha Naibu Waziri huyo aliagiza NOSC kueneza utaalum wa kuendeleza zao la chai katika mikoa mingine ili kuliendeleza kwani ardhi nzuri ya kilimo cha zao hilo ipo katika maeneo mbali mbali hapa nchini hivyo ni jukumu la wadau katika kuendeleza.

“Serikali itaendelea kushirikiana na SAGCOT na wadau mbalimbali katika jitihada za kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuzalisha malighafi kwa tija  ambayo ndiyo chachu ya uanzishwaji wa viwanda,” alisema

Alisema kwa kushirikiana kwa pamoja tutaweza kutekeleza ASDP II kwa muda uliopangwa na pia kufanya azma ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025 kufikiwa kwa vitendo kwani njia ya kuelekea katika mafanikio imeshaanza kupitia SAGCOT.

“Niwaombe SAGCOT kuwashirikisha vijana wajikite katika sekta ya kilimo kwani ndiyo kwenye uhakika mkubwa ajira , hivyo ni muhimu vijana wakahusishwa zaidi ili kupunguza wimbi la vijana kukosa ajira na badala yake wakajikita zaidi kwenye sekta ya kilimo,” alisema Naibu Waziri Bashungwa

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT,Bw.Geoffrey Kirenga alishukuru ujio wa Naibu waziri huyo na taarifa ya utendaji kazi wa Kituo  na mipango ya kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo nchini kwa kuanza na ukanda wa nyanda za juu kusini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za juu kusini mwa Tanzania (SAGCOT) Bw.Geoffrey Kirenga (katikati) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Kilimo Innocent Bashungwa  juu ya majukumu ya kituo chake katika kuinua sekta ya kilimo nchini. Kulia ni Mtaalam wa Sera wa SAGCOT,Bw.Prudence Lugendo



“Ujio wa mheshimiwa naibu wazirin umekuwa  ni faraja kwetu kwani ameweza kufahamu dhumuni la kituo chetu na zaidi ameweza kutoa mapendekezo na maagizo ambayo kama SAGCOT tumeyapokea na tutakwenda kuyatekeleza kikamilifu,” alisema Bw.Kirenga.

Alisema mapendekezo yake yote yatafanyiwa  kazi lengo likuwa kuboresha huduma katika kukuza na kuendeleza kilimo nchini kwa kumwinua mkulima mdogo kwa kushirikana na wadau na watoa huduma mbalimbali za kilimo.

SAGCOT ambayo imefanikiwa kuwaunganisha wakulima wadogo na kuwajengea
uwezo kupitia mafunzo mbalimbali imeshazindua kongani tatu mpaka sasa ambazo ni Ihemi inayoshughulikia mikoa ya Iringa na Njombe, Kongani ya Mbarali kwa mikoa ya Mbeya na Songwe na pia kongani ya Kilombero kwa Mkoa wa Morogoro na wilaya zake zote.

Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

Mbeya agro-processors get 5 acres to build 50 industries

Tanzania praised for being keen on fertilisers going to farmers

Mavunde: TADB offered 1.8bn/- to nurture Farm Access