NEMC yaeleza mafanikio ya kikosi kazi cha dharura
Na Paul Mahundi, Dar es Salaam
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema katika kipindi cha miezi minne ya uhai wa kikosi kazi cha dhararu kero na malalamiko juu ya uhifadhi wa mazingira vimepungua na Watanzania wamejenga tabia ya kuona mazingira yanatunzwa na kulindwa.
Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, ameeleza Jijini jana kwamba uanzishaji wa kikosi cha dharura kinachofanyakazi saa 24 umekuwa na manufaa kwa taifa kwa sababu wanachi wamepata mahali pa kupeleka taarifa na zikafanyiwa kazi.
“Hapo awali kulikuwa na malalamiko mengi kuhusiana na utiririshaji wa maji taka kutoka katika baadhi ya viwanda kwenda sehemu zisizohusika na wakati mwingine kwenye makazi ya watu. Lakini baada ya kuunda kikosi hiki kero zimepunguza sana hasa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam,’’ ameeleza Dkt. Gwamaka.
Amesema mbali na kudhibiti utiririshaji wa maji taka kwenye maeneo yasiyoruhusiwa, kikosi kazi kimesaidia kudhibiti uchimbaji wa mchanga kando kando ya mito, kuthibiti uchafuzi wa kelele pamoja na ukataji miti kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.
“Taarifa ambazo zimewasilishwa kwenye kikosi kazi zimesaidia sana kuchukua hatua za kudhibiti uchafuzi wa kelele, ukataji miti katika maeneo yasiyoruhusiwa na uchimbaji wa mchanga kando kando ya mito jambo linalochochea mafuriko na ubomokaji wa kingo za mito,’’ ameeleza. Tayari NEMC imezihimiza halmashauri za wilaya kuhakikisha vijana wanahamasishwa kuunda vikundi na kuvisajili ili uchimbaji mchanga uratibiwe na halmashauri zipate ushuru.
Amesema udhibiti na uimarishaji wa tabia ya usafi wa mazingira katika makazi ya watu na mito vimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, hasa katika maeneo yenye watu wengi kama Jijij la Dar es Salaam.
Dkt. Gwamaka amewashukuru wananchi na wadau wote wa mazingira kwa kushirikiana vizuri na baraza katika kufanikiisha malengo yake. “Tunawaomba wananchi wazidi kutoa ushirikiano ili kwa pamoja tuyafanye mazingira yetu kuwa bora na salama,’’ alisema.
Dkt Gwamaka amewakumbusha Watanzania kuzingatia Sheria ya Mazingira na Kanuni zake ili kuepuka migogoro ya kisheria inayoweza kutokea iwapo sheria na kanuni vitakiukwa na baraza likachukua hatua kwa wahusika.
“Baraza litaendelea kusimamia sheria na halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayekiuka sheria na kanuni zake. Nawaomba Watanzania wafuate sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa na wataalam wa mazingira ambao wanapatikana karibu nchi nzima,’’ alisema.
Comments
Post a Comment