Wakulima waimwagia sifa BriTEN kwa tiba ya udongo
David Nawepa, Iringa
Shirika
linalohudumia wakulima kuinua kupato chao la BriTEN limesifiwa na wakulima
wakati wa kozi mahususi ya kuwafunza wakulima namna ya kutumia chokaa mazao
kutibu udogo.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima, Bwana
Samuel Bangi, amewambia washiriki wa kozi hiyo kuwa awali wakulima walidhani
kuchoka kwa udongo ni jambo la kiasili ambalo linatokea kwa sababu tu ya
upandaji wa mimea wa mara kwa mara. Kwa
sababu ya imani hii, ameeleza, matokeo
yake wakulima waliendelea kuumia pasipokujua namna ya kujinasua.
“Tulikubaliana na mavuno kidogo au kuyakosa
kabisa kwa sababu hatukuja la kufanya na huku tunaumia,” amewambia wananchi waliohudhuria hafla hiyo.
Baada ya kuwaeleza wataalamu wa BriTEN,
ameeleza Bw Bangi mwenye shamba la darasa
katika kijiji cha Mlingano, jibu
lilipatikana.
“Hawa wataalamu kutoka BriTEN ndiyo
waliotusaidia kujua ukubwa wa tatizo; walileta
vifaa vyao wakaupima udongo na kutuelez una tindikali nyingi. Hivyo tukaanza kutumia chokaa mazao na
matokeo yake ni mazuri.”
Mapinduzi haya katika kutibu udongo
yamejitokeza katika ukuuji wa pato la wakulima kinyume na ilivyokuwa zamani.
“Mimi nimejenga nyumba mpya kutokana na
mavuno mazuri niliyoyapata baada ya kuanza kutumia huu utaalamu mpya,” amesema
Bw Bangi.
Naye Meneja wa Fedha na Uendeshaji wa
Kampuni ya Dodoma Cement, Bw Thomas Kohi, amewahakikishia wakulima wa Tanzania
kwamba kiwanda cha Dodoma Cement kina uwezo wa
kuzalisha chokaa mazao inayohitajika
kutibu udogo ulioathiriwa na tindikali.
“Hivyo msiwe na wasiwasi chokaa mazao ipo ya kutosha na imethibitishwa
na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na tumepewa hati.”
Amewambia wakulima kwamba pasipo kutibu
udongo ni kazi bure kuweka bidii katika kulima, kupanda na kutumia mbolea.
“Ni lazima udongo utibiwe kwa kutumia
chokaa mazao hadi kufikia daraja la PH 7, ndipo mbolea itaanza kufanya kazi.”
Ameeleza kuwa kiwanda kina uwezo mkubwa
wa kuzalisha chokaa mazao kwa wingi na kwamba iwapo mteja ataeleza mapema
mahitaji yake kiwanda hicho
kinaweza kuzalisha hata tani 100
kwa siku.
Amewahakikishia wakulima kwamba tani
moja ya chokaa mazao wataweza kuipata kwa shilingi 120,000/-
Hadhara hiyo ilitokana na ziara ya
kimafunzo kwa wakulima wa mahindi iliyoandaliwa
kwa pamoja kati ya Kituo cha Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu
Kusini (Sagcot) na Kampuni ya BriTEN katika kijiji cha Kiponzelo, mkoani hapa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya
BriTEN amesema kwamba amewaahidi wakulima hao ushirikiano zaidi na kwamba huu
ni mwanzo wa kunufaika na ushirikiano uliopo.
“Tumekuwa
karibu na wakulima hawa kwa muda mrefu.
Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha wanaelewa fursa zilizomo katika
kilimo, hasa kilimo cha mahindi ambacho
ni maarufu katika eneo hili. Kumekuwa na malalamiko ya kukosa mavuno ya
kutosha. Lakini baada ya kuupima udongo
tukabaini una tindikali nyingi. Hivyo huu ni mwanzo tu; tutawapa elimu na wakulima wa maeneo mengine
ili tatizo hili liishe kabisa,” amesema Bi. Kaiza.
Amebainisha
kuwa wameanza na wakulima wa kijiji hicho kwa kuwafunza namna ya kutumia chokaa
mazao. Baadaye, ameahidi, wataendelea na vijiji vingine kwenye kongani
hiyo ya Ihemi inayojumuisha mikoa ya Iringa na Njombe.
Naye Mkuu wa
Maendeleo ya Kongani kutoka Sagcot, Bi
Maria Ijumba, amewaomba wakulima wajifunze namna ya kutibu udongo kwa sababu
hilo ndilo suala la kwanza kabla ya kunza kupanda mazao.
“Afya ya udongo ndiyo suala la kwanza katika kupata mazao mengi na yenye
ubora hasa katika zama hizi ambazo kilimo kimekua biashara… Udongo ukikosa afya
hata tija katika mavuno inapungua,” amesema Bi. Ijumba.
SAGCOT ni
waunganishi wa sekta binafsi na sekta ya umma katika kutambua fursa kwenye
kilimo na kuongeza mnyororo thamani wa mazao ya mahindi, soya, nyanya, viazi
mviringo na maziwa katika kongani sita zilizopo ukanda wa nyanda za juu kusini
ikiwemo kongani ya Ihemi.
Kongani
za Sagcot ni Ihemi inayojumuisha mikoa ya Iringa na Njombe, Mbarali (Mbeya),
Sumbawanga (Rukwa), Ludewa (Ruvuma), Kilombero (Morogoro) na Rufiji (Pwani).
Comments
Post a Comment