TADB yatoa 1.8bn/- kufanikisha uzalishaji kiwanda cha Farm Access
Na Paul Mahundi, Dodoma
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Bw. Antony Mavunde ameeleza jinsi Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ilivyofanikikisha uzalishaji wa kiwanda cha
kutengeneza madawa ya mifugo cha Farm Access kwa kutoa shilingi 1.8bn/-.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitembelea maonesho
ya NaneNane katika Viwanja vya Nzuguni Jijini hapa jana na kufika banda
la Kiwanda, Waziri Mavunde alipongeza juhudi zinazofanywa Benki ya Kilimo na
hasa kufanikisha maendeleo ya sekta ya viwanda ikiwemo kiwanda cha Farm Access
kilichopo mkoani Dodoma.
“Naomba nichukue nafasi hii kuipongeza TADB na uongozi
wake kwa hatua stahiki na madhubuti kuunga mkono azma ya Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kujenga uchumi wa
viwanda hapa nchini” alisema Waziri Mavunde.
Alisema benki ilitoa fedha kwaaji ya ujenzi wa kiwanda mpaka
uzalishaji wake kuhakikisha utengenezaji na upatikanaji wa kutosha wa
madawa ya mifugo kiwandani hapo pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania.
Hatua hii ya kufanikisha ujenzi wa viwanda vya kimkakati
kama hiki cha Farm Access zitasaidia sana kupunguza changamoto za madawa
zinazowakabili wafugaji na wakulima sambamba na kuchochea ukuaji wa soko la
ajira, alisema.
Mbali ya kuvutiwa na bidhaa za kiwanda hicho, Waziri Mavunde
alimhakikishia Afisa Mwandamizi wa Maendeleo wa Kiwanda, Dkt. Simon
Mphuru kuwa serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kujenga uchumi unaotegemea
viwanda ifikapo mwaka 2025 na kuahidi kukitembelea kiwanda hicho siku chache
zijazo.
“Juhudi kama hizi lazima ziungwe mkono kwani zinalenga kuongeza
mapato ya serikali kupitia kodi na pia kuzalisha ajira kwa vijana wa kitanzania
sambamba na kuunganisha mazao ya wakulima katika mnyororo wa thamani”
alisema.
Aidha, Bw. Mavunde aliitaka TADB kuendelea kushirikiana na
mabenki washirika kwa kuwawezesha wakulima wa zao la zabibu kumiliki viwanda
vidogo vidogo vya kuongeza thamani ya zao hilo.
“Hatua za makusudi zinazochukuliwa na TADB kwa wakulima wa
zabibu zinapaswa kupongezwa na kila mpenda maendeleo wa nchi hii.Nina waomba
waendelee kuwajengea uwezo na kuwawezesha wakulima wadogo kumiliki
viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawasaidia kuongeza thamani ya zao hilo”
alisema.
Kwa upande wake, Dkt. Mphuru alimweleza Waziri Mavunde kuwa
kiwanda kitaendelea na uzalishaji na kuiomba TADB kuendelea kuwawezesha na
kuwajengea uwezo wakulima wadogo ili kufanikisha azma ya ujenzi wa
uchumi unaotegemea viwanda.
“Tunaishukuru TADB kwa mchango wake mkubwa katika kuleta mageuzi
na mafanikio katika sekta za kilimo na viwanda. Tunawahamasisha watanzania
wengi kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya kilimo”, alisema
Dkt. Mphuru.

Comments
Post a Comment