TPSF yaguswa bajeti ya mwaka 2020/2021

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta  Binafsi nchini( TPSF),Bi. Angelina Ngalula akizungumza kwenye mkutano na  waandishi wa habari jijini Dar es salaam mwishoni wa wiki juu ya  namna walivyoipokea Bajeti  ya Mwaka 2020/21 ambayo  imejikita zaidi  kupunguza gharama za  uzalishaji, kufanikisha utekelezaji wa Blue Print pamoja na kulinda Wiwanda vya ndani.

Na Abdallah Luambano, Dar es Salaam

TAASISI ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), imeipongeza Bajeti ya mwaka 2020/21 ambayo ilisomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango hivi karibuni kwa kujielekeza zaidi katika kupunguza gharama za uzalishaji, kufanikisha utekelezaji wa ‘Blue Print’ pamoja na kulinda viwanda vya ndani.

Akizungumza na  waandishi wa habari  jijini  Dar es salaam mwishoni mwa wiki kuhusu  bajeti hiyo iliyowavutia watu wengi,  Mwenyekiti wa TPSF, Bi. Angelina Ngalula mbali ya kuipongeza  serikali kwa kuja na bajeti hiyo, amesema  imegusa  maeneo mengi muhimu katika sekta mbalimbali za uchumi na kujikita zaidi katika kuinua maisha ya watanzania.

“Katika bajeti hii tumeona serikali imeanisha vipaumbele vyake katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa kutoa asilimia 37 ya bajeti kitu ambacho kitachochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya viwanda, uzalishaji na ajira na hatimaye kujenga uchumi imara na endelevu,’’ alisema Bi. Ngalula.

Bi. Ngalula alisema kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi unategemea uwepo wa taasisi binafsi ambayo hutafsiri yaliyomo kwenye bajeti kwenye maisha ya kawaida, hivyo amewataka wadau wa sekta hiyo kutumia mazingira hayo mazuri kuzidi kufanya biashara na kuwekeza zaidi.

“Unafuu wa kodi na kufutwa kwa tozo mbalimbali kunafanya mazingira ya biashara na uwekezaji kuwa katika hali nzuri, hivyo natoa wito kwa wawekezaji wazawa kutumia fursa zilizoainishwa katika bajeti hii ili kukuza mitaji yao, kuongeza mzunguko wa biashara na kutengeneza ajira kwa watanzania,’’ alisema.

 Aidha Bi. Ngalula alisema kuwa bajeti hiyo imeonesha mwanga kwa taifa kupunguza hali ya utegemezi katika kushughulikia masuala ya ndani ya uchumi wa nchi hasa katika kipindi hiki ambacho dunia nzima inapambana na janga la ugonjwa wa COVID-19.

“”Serikali kupitia Rais Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa ikihimiza umuhimu wa kujitegemea na hasa kipindi hiki ambacho ugonjwa wa COVID-19 umeikumba dunia. Wito wangu kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani kuitafsiri dhana ya kujitegemea kwa vitendo katika maeneo ya vifaa tiba/kinga, usarishaji wa anga wa mizigo, chakula na kuzalisha malighafi za viwandani,’’ alisistiza Bi. Ngalula.

Mbali ya hilo Bi. Ngalula ameongeza kuwa  hatua ya serikali kupendekeza kutolewa kwa tozo 60 za udhibiti kutarahisisha zaidi shughuli za ufanyaji biashara na uwekezaji.

“Kilio cha wafanyabiashara na wawekezaji  ni uwepo wa tozo nyingi ambazo zilikuwa kikwazo, kuondolewa kwa tozo hizo 60 kutasaidia wadau wa maendeleo kujihusisha zaidi na uwekezaji na biashara hali ambayo itachangia ukusanyaji wa kodi na kutengeneza ajira kwa vijana wa kitanzania,’’ alisema na kuongeza TPSF itaendelea kuwa kuwaanganisha wadau wake na serikali ili kufikia azma ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.




Comments

Popular posts from this blog

Kirenga: Kipaumbele chetu ni mkulima mdogo kupata soko la uhakika

Kigamboni gets world class secondary school

TADB-supported projects for Uhuru call