TPSF yapongezwa kuhusu angalizo ajira
Na Mosses Ferdinand, Dar es Salaam
WAFANYAKAZI hapa nchini wamepongeza angalizo lililotolewa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kwa waajiri kuwa maambukizi na kuenea kwa Virusi vya ugonjwa wa COVID-19 lisichukuliwe kama kisingizio cha kuwaachisha kazi wafanyakazi kiholela.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyakazi
wengi wamepongeza hatua ya Taasisi hiyo kutoa angalizo mapema kabla ya kuenea
maambukizi mengi kwani waajiri wengi wasiowaaminifu hupenda kutumia majanga
mbalimbali kupunguza wafanyakazi kama hatua ya kupambana na athari za kutokea janga.
 “Kama mfanyakazi nimefarijika
sana  na tamko au angalizo la TPSF na kuungwa mkono na chama cha waajiri Tanzania
(ATE)kuwa wapo waajiri wengi katika sekta binafsi watakaotumia mlipuko wa
COVID-19 kama sababu ya kupunguza au kubana maslahi ya wafanyakazi,’’ alisema
Seif Almas mfanyakazi wa kiwanda wa kimoja cha kutengeza mifuko mbadala jijini
Dar es Salaam jana.
Bi. Neema Joram ambaye ni mfanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ujenzi eneo la Mikocheni na ambaye hakuwa tayari kutaja jina la mwajiri wake, alisema angalizo limetolewa wakati mwafaka huku serikali kupitia Wizara ya Afya ikiendelea kutoa muongozo wa kujikinga na katua mbalimbali zinazochukuliwa kukabiliana na maambukizi kuenea hapa nchini.
“Angalizo la TPSF kwa waajiri siyo
kwamba linaleta ahueni kwa wafanyakazi tu bali hata nchi kwa ujumla ambayo
imekuwa ikipata kodi kupitia mishahara ya wafanyakazi, viwanda, mashirika na
taasisi mbalimbali,” alisema Bi Neema na kuwataka watanzania kufanyakazi kwa bidii
na kuzingatia kinga dhidi ya maambukizi.
Hivi karibuni, TPSF iliandaa mkutano na vyombo vya habari kuelezea dhamira yake ya dhati kuunga mkono na kuipongeza serikali ya awamu ya tano kwa hatua na mikakati madhubuti iliyochukua mpaka sasa kukabiliana na maambukizi ya Corona.
Mkutano huo ambao uliongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Bi Angelina Ngalula aliwaonya waajiri hapa nchini kuchukua tahadhari ya maambukizi ya Corona na kwamba kusiwe na visingizio vya kupunguza wafanyakazi kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo sehemu mbalimbali duniani.
Alisema TPSF imeunda Kamati Maalumu kushughulikia suala la Corona ambapo imejielekeza zaidi katika mambo makuu matatu ikiwepo kutoa elimu ya kutosha kwa jamii kwa mujibu wa muungozo na maelekezo ya serikali kupitia Wizara ya Afya.
“Kamati inafanya kazi pia kuhamasisha uchangiaji wa rasilimali vifaa kwaajili ya kukinga kuenea maambukizi hayo kupitia Kongani zake 14 chini ya mwamvuli wa taasisi,” alisema Bi Ngalula na kuongeza kuwa pia kamati itafanya tathmini ya athari za kiuchumi na kijamii
zitatakazotokana na Corona hapa Tanzania.
Katika Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk Aggrey Mlimuka licha ya kupongeza angalizo hilo, aliiomba serikali kuzidi kuchukua hatua zaidi kwa kuondoa baadhi ya tozo zisizo na ulazima ili kulinda ajira.
“Upande wa ajira bado athari zake hazijawa kubwa sana, tunawapongeza TPSF kwa angalizo lao ambalo litawafanya waajiri kuwa makini na kuweka mipango zaidi kwenye taasisi na kampuni zao ili kulinda ajira,” alisisitiza.
Mwisho.
Comments
Post a Comment