TPSF yaainisha vipaumbele vyake vita dhidi ya kukabiliana Corona
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi.Angelina Ngalula akijadiliana jambo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC),Dkt. Godwill Wanga(katikati) mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari uliolenga kuelezea hatua zilizochukuliwa na TPSF katika kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayotokana na virusi vya COVID 19 kwa kuhakikisha uwepo wa usalama wa biashara na ajira kwa watanzania. Kulia ni Mjumbe wa Kamati iliyoundea na TPSF kushughulikia athari za ugonjwa huu,Bw.Karim Premji.
|
Na Isdory Njavike, Dar es Salaam
KATIKA juhudi za kuhakikisha kuwa maambukizi ya ugonjwa wa Corona hauenei na kuleta madhara katika sekta mbalimbali za uchumi hapa nchini, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeunda kamati maalum ya kushughulikia suala hilo sambamba na vipaumbele vyake vya tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TPSF, Bi Angelina Ngalula amesema sekta binafsi imeguswa na kutambua kazi kubwa inayofanywa na serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo na hivyo sekta binafsi haina budi kuunga mkono juhudi hizo kwa vitendo.
“Tunapenda kutambua jitihada za Rais Dkt John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya Bi Ummy Mwalimu kwa kuweka mikatiti mahususi ya kupambana na ugonjwa huu na kuhakikisha tunajiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa kiafya, kijamii na kiuchumi,” alisema Bi Ngalula.
Bi Ngalula amesema TPSF kupitia kamati yake imejipanga kutoa elimu kwa umma kuhusu maambukizi, kujikinga na kudhibiti ugonjwa huo kulinga na muongozo na maelekezo yaliyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya.
“Taasisi itashirikiana na wadau wa sekta kuhakikisha jamii ya Tanzania inapata taarifa sahihi katika maeneo yote matatu yaani maambukizi,kujikinga na kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo,” alisema na kuongeza kuwa Kamati ilishakutana na Waziri wa Afya na Naibu wake. Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kazi ya pili ya kamati hiyo itakuwa kushirikiana na wadau kufanya uhamasishaji wa upatikaji wa raslimali zinazohitaji katika kudhibiti maambukizi na athari za ugonjwa
“Pamoja na mambo mengine, kamati iliyozungumza na Waziri Mwalimu na Naibu wake Dkt. Faustine Ndungulile kuhusu vifaa vinavyohitajika kama vilivyoainishwa na Waziri wa Afya ni pamoja na (masks, sanitizers, protective gowns, ventilators, ambulance, scanners kama walk-through scanners na oxygen materials,” alisema.
Bi Ngalula aliitaja kazi ya tatu ya kama hiyo ni kulinda ajira za watanzania ambapo alisema TPSF kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameshaanza kujadili na kupanga mikakati ya kuona namna bora ya kulinda ajira za watu, biashara na uzalishaji.
“Tunapenda kuunga mkono taarifa aliyoitoa Mheshimiwa Rais (jana)jumapili kupitia vyombo vya habari kuwatoa hofu watanzania na kuwaomba waendelee na kazi huku wakichukua taadhari ziwekwa za kujikinga na ugonjwa huo,” alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu kamati hiyo, Bi Ngalula alisema mpaka sasa TPSF kupitia kamati yake imeshafanya mambo mengi ikiwemo kuanza zoezi la kufanya tathmini ya awali ya athari za COVID-19 kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi.
“Tayari wadau mbalimbali wa sekta binafsi wameshatoa majengo kwa ajili ya kuwahifadhi baada ya wasafiri wenye mambukizi kama sehemu ya kujitenga kwa muda wa wiki mbili inayojulikana kama self-isolation,” alisema.
Bi Ngalula alisema kwa upande wa Wamiliki wa Malori Tanzania(TATOA) wamehamasisha wananchama wake kutoa elimu ya maambukizi, kinga na udhibiti wa ugonjwa huo kwa madereva na wasaidizi wao.
“Tumeshahamasisha viongozi wote wa kongani 14 za taasisi kutoa elimu kwa wanachama wao katika kongani husika juu ya ugonjwa huo sambamba na muungozo wa wizara ya Afya,” alisisitiza.
Mwisho.
Comments
Post a Comment