Ngalula: Tusitumie Corona kupunguza wafanyakazi


Na Jackson Kulinga Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Angelina Ngalula,  ameasa wanachama wa taasisi hiyo wasitumie ugonjwa wa Corona  kupunguza wafanyakazi katika viwanda au kampuni wanazozimiliki.

Amewambia waandishi wa habari hapa jana kwamba Tanzania na dunia kwa jumla vinapita katika kipindi kigumu kutokana na ugonjwa wa corona, lakini akaongeza kuwa siyo busara   kutumia tatizo hilo kupunguza wafanyakazi.

“Kupunguza wafanyakazi  litakuwa ni tatizo kubwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Hivyo nawaomba waajiri kote nchini tushughulikie changamoto zilizopo kwa pamoja ili kulinda ajira nchini.  Kutumia matatizo kujinufaisha siyo utamaduni wa Watanzania,’’ amekumbusha Bi. Ngalula.

Amesema kongani, mfano Utalii na Kilimo,  ambazo zimeathirika moja kwa moja kutokana na ugonjwa wa corona  zikusanywe taarifa zinazoonesha namna mtu mmoja mmoja alivyoathirika na taarifa hizo ziwasilishwe kwenye kikosi kazi ambacho tayari kimeundwa.

‘’Taarifa hizo zitachambuliwa  wataalamu wetu na kufikishwa serikalini. Msitengeneza makundi yenye lengo la kujinufaisha.’’ ameeleza Bi. Ngalula na kuongeza kwamba jambo muhimu ni kuendelea kufanya kazi kama ambavyo Rais John  Magufuli amewaomba Watanzania.

“TPSF tutaendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kufanya kazi na kuongeza tija kwa taifa lakini lazima kuchukua hatua zinazofaa katika maeneo ya kazi ili kuwalinda wafanyakazi wasipate maambukizi ya virusi vya Corona,’’ amesema.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk Aggrey Mlimuka, amesema huu si wakati muafaka kwa watu kufungiwa ndani kwani athari zake zitakuwa kubwa kwenye  ajira na  uchumi wa nchi utaporomoka.

“Zipo nchi zimefunga ofisi zote za umma na binafsi kukabiliana na ugonjwa wa Corona.  Sisi kama Chama cha Waajiri tunaunga mkono kauli ya Rais John Pombe Magufuli inayowataka Watanzania kuendelea kufanya kazi huku tahadhari za kukabiliana na Corona zikiendelea kuchukuliwa,’’ amesema  Dk. Mlimuka na kuiomba serikali kuondoa baadhi ya tozo kwa taasisi au kampuni zitakazoathiriwa na ugonjwa wa Corona.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk. Godwill Wanga, amewataka wafanyabiashara kuacha ubinafsi na kufikiria maslahi mapana ya nchi badala ya kutumia matatizo ya corona kujinufaisha.

“Wote tunafahamu kwamba dunia nzima inapambana na virusi vya corona. Tanzania bado hali haijawa mbaya sana na tunaomba tusiathirike zaidi. Kutumia janga la corona kupunguza ajira ni kuhatarisha uchumi wetu. Tuwe wawazi na kuelekeza changamoto zetu katika maeneo husika ili kunusuru uchumi,’’ amesema Dk. Wanga.

Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

Set aside land for investment, Kairuki tells RCs,district councils

NEMC warns on emptying effluent in built-up areas, flood waters

TADB-supported projects for Uhuru call