Simbachawene aitaka NEMC kudhibiti usafirishwaji chuma chakavu mipakani
| Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, George Simbachawene (kulia) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu Wa NEMC Dkt, Samwel Gwamaka(kushoto) alipofanya ziara katika Bandari ya Dar es salaam kukagua makontena yenye vyuma chakavu ambayo yalikuwa tayari kusafirishwa nje ya nchi na kutoa agizo la kusitisha biashara ya usafirishwaji wa vyuma chakavu nje ya nchi. |
Simbachawene aitaka NEMC kudhibiti usafirishwaji chuma chakavu mipakani
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Bw.
George Simbachawene amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira (NEMC), kutumia ofisi zake za kanda kudhibiti
usafirishwaji wa chuma chakavu maeneo yote ye mipaka.
Akizungumza mwishoni mwa wiki mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya
siku moja ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam kujionea namna
zoezi la usafirishaji wa chuma chakavu inavyoendeshwa, Waziri
Simbachawene hakuridhishwa na utaratibu unaotumika sasa kusafirisha
chuma chakavu kwani unachangia upotevu wa mapato ya serikali.
“Biashara hii inafaida kubwa kwa wafanyabiashara na utaratibu
unaotumika sasa kusafirisha chuma chakavu hauisaidii serikali kupata
mapato kupitia kodi kwa kuwa hakuna utaratibu wa kutoa risiti,”
alisema Waziri Simbachawene.
Waziri alisema kuwa katika kipindi hiki ambapo azma ya serikali ni
kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025, chuma chakavu ni moja
ya malighafi muhimu zaidi kwa viwanda vya hapa nchini.
“Chuma chakavu ambavyo inaruhusiwa kusafirishwa nje ya nchi ni ‘cast
iron’ lakini vyuma vingine vyote lazima vibaki hapa nchini kwani hata
viwanda vya ndani vimekuwa na uhitaji mkubwa wa chuma hivyo,” alisema
na kuongeza kuwa NEMC lazima wajipange kudhibiti usafirishaji wa chuma
chakavu.
Simbachawene mbali ya kuiagiza NEMC kutumia ofisi zake za kanda
aliwataka pia Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusaidia kudhibiti usafirishaji
wa chuma chakavu katika maeneo yao na hasa mipakani ilikuzuia upotevu
wa mapato ya serikali.
Aidha Waziri ametoa muda kwa mamlaka husika kutoa maelezo ya kina juu
ya makontena 18 ya chuma chakavu iliyosafirishwa nje ya nchi licha ya
kuwepo kwa zuio la kusafirishwa makontena hayo.
“Mamlaka zote zinazohusika na ukaguzi wa chuma chakavu kabla
havijasafirishwa zikae pamoja na zije na majibu ya kwa nini makontena
18 yamesafirishwa licha ya kuwepo na zuio la kutosafirishwa, chuma
chakavu ni biashara kubwa sasa pengine kuliko hata madini,”
alisisitiza Waziri Simbachawene.
Kwa upande wake Meneja wa Forodha Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Njaule
Mdendu alisema kuwa ziara ya Waziri imetoa mwanga mpya katika
kusimamia usafirishaji wa chuma chakavu na kuahidi kufanyia kazi
changamoto zake.
“Tunamshukuru Waziri kwa namna alivyotoa ufafanuzi kwa baadhi ya mambo
hali ambayo itaongeza ufanisi, lakini hata hivyo uwepo wa maofisa
wakazi wa NEMC unaweza kusaidia katika kutoa elimu na kufanya ukaguzi
wa chuma gani inapaswa kubaki na vipi vinapaswa kusafirishwa nje ya
nchi badala ya kuja na kuondoka,” alisema Bw. Mdendu.
NEMC wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha usafirishaji wa vyuma
chakavu unafuata sheria na kanuni zilizopo ili zisilete athari katika
mazingira na sasa wametakiwa kwenda mbali zaidi ya hapo kwa kuangalia
ni chuma zinazopaswa zinazopaswa kusafirishwa na vipi havitakiwi
kusafirishwa kwani viwanda vya ndani navyo vimekuwa na uhitaji wa
malighafi hiyo.
Mwisho.
Comments
Post a Comment